WIVU ANAOUTAKA BWANA

Biblia kwa kina No Comments

WIVU ANAOUTAKA BWANA

Jina kuu tukufu la Bwana Yesu Kristo Mkuu wa wafalme wa dunia libarikiwe milele na milele.

Karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu.

Siku ya leo kwa neema za Bwana, tutajifunza wivu anaoutaka Bwana tuwe nayo, nikisema wivu anaoutaka Bwana maana yake kuna wivu asioutaka.

Sasa kabla hatujafahamu wivu anaoutaka Bwana, hebu tufahamu wivu asioutaka.

Bwana Mungu alivyomuumba mwanadamu..alimuumba kwa mfano wake na kwa sura yake.

Mwanzo 1:26-27 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

[27]Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Kwa mfano wake maana yake ni ule utu wa ndani ambayo ndiyo inabeba hisia kama upendo, hasira, wivu, huzuni n.k na kwa sura yake(muonekano wa nje).

Kwahiyo kama tumeumbwa kwa mfano wake na kwa sura yake.. maana yake tabia na muonekano aliyonayo Mungu na sisi tunazo.

Kwa mfano, ukimuangalia mwanadamu utamwona na tabia kama vile upole, ukali, upendo, chuki, huzuni, furaha, hasira, hofu, wivu n.k, sasa hizi tabia sio kwamba amezaliwa akazikuta duniani au akajifunza, hapana, bali alizaliwanazo kwasababu aliumbwa kwa mfano wa Mungu, ikiwa na maana Mungu pia anazo tabia kama hizo. Kwa mfano ukisoma biblia utakuta sehemu nyingine Mungu anasema yeye ni Mungu mwenye wivu ikiwa na maana anayo wivu kama  tulivyo na sisi.

Kutoka 34:14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.

Kadhalika na sehemu zingine Mungu anaonesha kuwa na tabia kama hasira, upendo, huzuni, kama tulivyo na sisi.

Nahumu 1:2 BWANA ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; BWANA hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira.

Sasa utauliza, kwahiyo kuwa na wivu, hasira, chuki, sio dhambi?

Jibu ni ndio sio dhambi, isipokuwa tabia hizo zikitumika vibaya zinageuka kuwa dhambi.

Hebu tuone moja ya tabia ambayo ikitumiwa vibaya inakuwa ni dhambi kwa Mungu.

Wivu asioutaka Mungu

Kwa mfano mtu atamwonea mwingine wivu kwasababu kapata kitu fulani ambacho yeye hajakipata, hivyo atatamani au atatafuta njia yule mtu akipoteze kile kitu ndipo atulie.

Mfano wa wivu huu ni ule aliokuwa nao Kaini, alipoona sadaka ya ndugu yake imekubaliwa na kwake imekataliwa. Badala atafute njia ya kuboresha sadaka yake ikubalike mbele za Mungu kama ya ndugu yake, yeye akatafuta kumwua ndugu yake, (wivu unaoishia kuleta chuki, masengenyo, vinyongo, visasi ni wa kishetani)..ambao ni dhambi mtu kuwa nao sawasawa na Wagalatia 5:20.

Wivu wa ki-Mungu

Wivu wa kiMungu ni ule unaomfanya mtu atamani kuwa mwema kama mwingine alivyo mwema, unaomfanya mtu atamani kufanya vizuri kama mwingine anavyofanya vizuri pasipo kumtakia madhara yule mwingine, (kwa ufupi haufurahii kuanguka wala kupunguka kwa mwingine)..zaidi sana mafanikio ya mwingine yanakuwa siku zote ni darasa kwake….

Wivu huu sio mbaya na si dhambi mtu kuwa nao, kwasababu matunda yake ni mazuri..

Mfano wa huu ni ule Mtume Paulo, aliojaribu kuutia kwa ndugu zake Waisraeli ili wamgeukie Mungu zaidi.

Warumi 11:14 “nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao”.

Lakini pia upo Wivu mwingine wa KiMungu ambao unaishia kuharibu vitu vya kishetani lakini si kimharibu mtu..

Mfano wa wivu huu ni alikuwa nao Bwana Yesu juu ya Hekalu la Mungu, alipoingia na kukuta watu wanafanya biashara ndani ya hekalu, maandiko yanasema Bwana alizipindua meza zao, na kuharibu biashara zao lakini si kuwaharibu wao.. Na wanafunzi wake wakakumbuka andiko la wivu wa nyumba ya Mungu utamla (Yohana 2:17).

Pia tunasoma kwa habari ya mtu mmoja aliyeitwa Finehasi mwana wa Haruni (kuhani) ambaye alikuwa na wivu kama huu ambao Bwana anataka na sisi tuwe nayo,

Finehasi alipoona mtu anamwingiza mwanamke ndani ya hema ili akazini naye tena mbele ya kusanyiko lote bila wasi wasi, wivu wa Mungu ulimjia, akaamka na kwenda kumuondosha kwa fumo lake, na Bwana akazuia lile pigo kwa sababu ya ile wivu aliyoonyesha Finehasi.

Hesabu 25:6-13 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania.

[7]Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;

[8]akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli.

[9]Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.

[10]Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia,

[11]Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, KWA KUWA ALIKUWA NA WIVU KATI YAO KWA WIVU WANGU MIMI, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu.

[12]Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani;

[13]tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; KWA SABABU ALIKUWA NA WIVU KWA AJILI YA MUNGU WAKE, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli.

Wivu huu pia na sisi tunapaswa tuwe nao tunapoona kazi ya Mungu inachafuka, ni lazima tusimame kuziharibu hizo kazi za shetani kwa maombi na kwa mafundisho sahihi, lakini si kwa kuwadhuru watu au kuwatukana, au kuwaletea madhara yoyote ya kimwili.

Je! unasumbuliwa na dhambi ya Wivu wa kidunia ambao unaishia kusengenya, kuona hasira, kuua, kutukana n.k Na hujui utatokaje katika hilo shimo?.

Bwana Yesu amekuja kwaajili ya kututoa katika hayo mashimo, kwa nguvu zetu hatuwezi kutoka huko wala kujitoa.

Nguvu pekee ya kututoa huko ni kwa njia kwa ya Roho Mtakatifu, kwa somo kamili kuhusiana na Roho Mtakatifu, jinsi ya kumpokea na jinsi atakavyokuwezesha kushinda yale usiyoweza kuyashinda basi tutumie ujumbe inbox ili uweze kupata somo hilo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *