
OLE WAO WAKUSUDIAO MAMBO MAOVU
Kuna watu wanakusudia kutenda mambo maovu wazi wazi..hata hawaogopi aliye juu. Lakini Bwana anasema itakuwa “OLE” kwa watu hawa.
Mika 2:1 “Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao”.
Kumbuka watu hawa wanakusudia kabisa wenyewe kwa akili zao, sio kana kwamba wamepitiwa bahati mbaya!! Hapana WANAKUSUDIA ndani ya mioyo yao wenyewe. Kwasababu tu wanao uwezo katika mikono yao, miguu yao, midomo yao, wanafanya hivyo, miili yao ikiwaka tamaa wanazini tu watakavyo, wengine wanajichua, wengine wanaiba, wengine wanakunywa kileo yeyote watakavyo, wengine wanavaa jinsi watakavyo, hakuna wa kuwaambia kitu. Kwa mfano kuna mtu mmoja aliniambia “nikilewa ni pesa yangu natumia” mwingine akaniambia acha kunifuatilia kwani anayekwenda kuhukumiwa ni mimi sio wewe”. Na wengine wanajifariji na kuendelea kufanya maovu gizani huku wakisema..Ni nani anayetuona, ni nani anayetujua. Lakini Bwana anasema…
Isaya 29:15 “Ole wao wanaojitahidi kumficha BWANA mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?
Ndugu, huwenda ni wewe leo umekutana na ujumbe huu, fahamu tu kuwa pamoja na kwamba kwa sasa hakuna jambo baya linalokupata unapofanya hayo mambo ambayo we mwenyewe unajua hayampendezi Mungu lakini umeamua tu kufanya, basi fahamu ya kuwa mwisho wa siku Mungu atakuleta tu hukumuni, huwezi kuukwepa biblia inasema hivyo..
Mhubiri 11:8-9 “Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Mambo yote yajayo ni ubatili.
[9]Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, LAKINI UJUE WEWE YA KWAMBA KWA AJILI YA HAYO YOTE MUNGU ATAKULETA HUKUMUNI.
We ni binti amua tu kuuharibu mwili wako kwa uasherarati, amua tu kujipodoa mwili wako na kutembeza uchi kwa kuvaa nguo za utupu, nguo za kubana, we ni kijana endelea kula ujana, endelea kujichua, endelea kukusudia kutenda mambo mabaya.
We usitake kuonywa, usitake kumsikiliza mtu yeyote, we endelea na uhuni wako, endelea kuiba, endelea na rushwa, endelea na ulevi, endelea na uchawi, endelea kujinenepesha na maovu hayo yote ili upate hukumu inayokustahili… maana biblia inasema
“Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa”. (Ufunuo22:11)
Hukumu ya jehanamu inatisha sana, ni heri leo uache kiburi chako na kuamua kuokoka kweli kweli. Kusudia leo kuanza maisha mapya ndani ya YESU KRISTO ili uokoke na hukumu ya jehanamu, kumbuka hakuna dhambi isiyowezekana kuacha ikiwa tu mtu amedhamiria kuacha kabisa. Wengi huwa hawafanyi hivyo, wanaenda kanisani na huku bado wanaishi katika dhambi, wenaenda kubatizwa lakini hawajaamua kuacha dhambi hilo ndilo tatizo la watu wengi. ndugu fahamu kuwa hakuna muujiza wa kuombewa ili uache dhambi…ni wewe mwenyewe kuamua KUACHA tu kwe vitendo kabisa na kumfuata Yesu, hapo ndipo Roho Mtakatifu atapata nafasi ya kukusadia kuendelea mbele.
Mungu akubariki.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Maran atha (Bwana Yesu anarudi)