UHAI WETU UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO.

Biblia kwa kina No Comments

UHAI WETU UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO.

Wakolosai 3:3 Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.

[4]Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”.

Jina la YESU KRISTO libarikiwe daima, karibu tujifunze Neno la Mungu taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Mtu anapotii injili ya Kristo na kuamua kumgeukia Kristo akabatizwa kwa maji na kwa Roho, mtu huyu anakuwa kiumbe kipya, anakuwa mwana wa Mungu mridhi wa baraka za Mungu, anakuwa amevuka mautini kuingia uzimani, uhai wake unakuwa umefichwa pamoja na Kristo hakuna mchawi yeyote au pepo lolote linaweza kumpata, wala hakuna laana za ukoo na mababu zitaweza kumfuatilia tena, hakuna roho yoyote chafu zitaweza kumsumbua, kwasababu gani? Kwasababu uhai wake umefichwa pamoja na Kristo.

Hivyo wewe uliye ndani ya Kristo..nikutie tu nguvu kuwa usitishwe na kitu chochote, wala usihofie zile ndoto unazoletewa kuwa unalogwa na watu fulani, au mahubiri yanayokuambia ukoo wenu unalaana hivyo huwezi kufanikiwa, wao ni wao na wewe ni wewe..haupo tena kwenye huo mnyororo wa wazazi wako. Uhai wako umefichwa pamoja na Kristo.

Lakini wewe uliye nje ya Yesu Kristo fahamu kuwa haupo salama hata kidogo, kwani bado upo kwenye miliki ya shetani, uhai wako haujafichwa pamoja na Kristo… hivyo shetani anaweza akakufanya lolote hata kukuua.

Sasa ufanyeje ili uhai wako ufichwe mbali na shetani??

Kwanza tunapaswa tufe kwa habari ya dhambi kwasababu kitendo hicho ni kitendo kinacholazimisha UHAI wetu kuhamishwa toka pale ulipokuwa kwanza na kwenda sehemu nyingine..

Kama vile tunavyojua siku zote kitu pekee kinachoweza kuuhamisha uhai wa mtu ni Kifo. Ukifa leo hii Moja kwa moja uhai wako unatoka na kwenda kwingine.., Na hiyo inapelekea watu kutokutujua mahali ulipoelekea, haijalishi watakutafuta vipi kamwe hawatakaa wajue mahali ulipo isipokuwa Mungu peke yake.

Na ndivyo ilivyo pale mtu anapokufa kwa habari ya dhambi, kwa kuzaliwa mara ya pili, Uhai wake unahamishwa na kwenda kuficha na Mungu mwenyewe, mbali na shetani au kitu kingine chochote, kiasi kwamba hata ibilisi akutafuteje rohoni hawezi kukupata kamwe…

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu”.

Unaona, pale tunapokufa ndipo uhai wetu unapofichwa. Ikiwa tutasema tumeokoka, lakini bado tunaendelea kuyaishi maisha yale yale ya kale, tuwe na uhakika kuwa Mungu hata hana shughuli na uhai wetu..Ikiwa hatutakuwa tayari kuacha uzinzi wetu, uasherati, disko, fashion, matusi, ulevi, ambayo tunafanya mara kwa mara n.k. basi tujue bado shetani anayo mamlaka makubwa sana juu ya uhai wetu..

Anao uwezo wa kututumia vyovyote apendavyo, anao uwezo wa kuyashinda maamuzi yetu, anao uwezo wa kutuletea majaribu ya ajabu ajabu, ikiwemo vifo visivyo vya wakati, anao uwezo wa kuyazuia maombi yetu, anauwezo wa kutufanya tusiyaelewe maandiko. Na zaidi ya yote anakuwa na uwezo wa kuyaingilia maisha yetu kwa viwango kikubwa sana kwa kwa kutumia majeshi ya mapepo yake.

Na ndio hapo utaona, mtu anasema siwezi kushinda dhambi Fulani, siwezi kuacha kuishi maisha Fulani ya dhambi, siwezi kuacha kujichua , Ni kwasababu hakukubali kufa kwanza ili uhai wake uchukuliwe na kwenda kufichwa kwenye moyo wa Mungu.

Mtu aliyefichwa uhai wake, shetani anakuwa haelewi chochote Mungu alichokipanga juu yake, shetani anachofanya ni ku-kisia kisia tu, pengine kesho yake itakuwa hivi au itakuwa vile, lakini haelewi chochote uhai wake unaendelea kuwa moyoni mwa Mungu mbinguni daima, umefichwa huko, ukisubiria wakati maalumu wa kufichuliwa tena.. Kwasababu kitu kinachofichwa ni sharti siku moja kifichuliwe/kifunuliwe.

Na utafunuliwa lini? Biblia inaendelea kusema..

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.

4 Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”.

Ipo siku ambayo, watu wote wa Mungu watafahamu kusudi halisi la Mungu kuwaumba ni nini?.. siku watakapoona mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, siku ambayo watakavikwa miili mipya isiyoharibika na kutawala na Kristo kama wafalme na makuhani milele.. Ni siku isiyokuwa na mfano, Hatupaswi kuikosa hata mmoja wetu.

Je! Uhai wako umefichwa pamoja na Kristo?? Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati kabisa na moja ya siku hizi parapanda italia na watakatifu watanyakuliwa, jiulize utakuwa wapi wewe siku hiyo ikiwa ni leo usiku au kesho asubuhi, una uhakika wa kwenda na Bwana??

Neema ya Mungu itusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *