TANGU SASA MTU ASINITAABISHE, KWA MAANA NINACHUKUA MWILINI MWANGU CHAPA ZAKE YESU.

Biblia kwa kina No Comments

TANGU SASA MTU ASINITAABISHE, KWA MAANA NINACHUKUA MWILINI MWANGU CHAPA ZAKE YESU.

Ninakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu karibu tujifunze neno la Mungu chakula cha roho zetu.

Wagalatia 6:17 “Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua MWILINI MWANGU chapa zake Yesu”.

Chapa za Yesu ni zipi? Kwanza ni vizuri kufahamu maana ya chapa, chapa ni alama..Chochote kilichopigwa chapa maana yake kimewekwa alama inayokitambulisha kitu hicho kuwa ni milki ya kitu kingine.

Sasa chapa za Yesu ni zipi? Si nyingine Zaidi ya zile za Mateso, makovu ya misumari katika mwili wake, makovu ya viboko katika mgongo wake, uso uliotemewa mate, msalaba juu ya mwili wake n.k. Hizo ndizo alama au chapa za Yesu. Na hapa Mtume Paulo anasema naye pia anazichukua katika mwili wake…zingatia hilo neno “MWILINI MWANGU” maana yake hizo ndizo zitakazomthibitisha kwamba yeye ni milki ya Yesu. Na sio vinginevyo, sio kuwa na jina lake tu (namaanisha kuwa na jina la Yesu) kwasababu hata walevi na wazinzi wanaweza wakawa na jina la Yesu wakaitwa wakristo.

Wengi hatupendi kusikia habari ya kupitia dhiki na kuudhiwa kwa ajili ya imani, kwasababu tunafikiri Ukristo ni kupata tu raha na burudani katika haya Maisha…Bwana Yesu alisema mtu yoyote akitaka kunifuata sharti ajitwike msalaba wake na ajikane nafsi yake ndipo amfuate…Maana yake huo msalaba atakaojitwika ndio utakaompeleka msalabani… msalaba alioubeba Bwana ulimpeleka kufa pale Kalvari kifo cha mateso…wewe na mimi ni misalaba gani tunayoibeba ambayo mwisho wa siku itatupekea kuifia Imani, au kuteswa kwa ajili ya Imani?..Misalaba unayovaa shingoni ni urembo tu.

Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; 

Soma tena 1Wathesalonike 3:3, 2Wathesalonike 1:4-5.

“.. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo”.(Yohana20:25)

Wengi tunadhani Tomaso alikuwa hatambui anachosema pale alipotoa matamshi kama hayo, lakini ukweli ni kwamba Tomaso alitaka kupata uhakika ya kuwa je! Huyu ndiye Yule YESU aliyesulibiwa msalabani au la?. Na tunaona alipomdhibitisha kuwa ndiye mwenyewe kwa zile ALAMA zilizokuwa mwilini mwake alimkiri na kusema “BWANA WANGU na MUNGU WANGU”

Maneno haya yanatufundisha kwamba USHAHIDI wa kwanza kama kweli tumeamua kumfuata YESU, ni lazima tutakuwa na misalaba migongoni mwetu, hii ikiwa na maana kuwa kama hatujaibeba misalaba yetu ni dhahiri kuwa bado hatuajaanza safari ya kumfuata, hata kama tunadai kiasi gani kuwa tunampenda YESU, au tunamwamini, au vyovyote vile hapo bado hatujamfuata mpaka siku ile tutakapochukua uamuzi wa kujitwika misalaba yetu na kuambatana naye.

Kumbuka msalaba ni kiashiria cha dhiki au mateso utakayopitia kwa ajili ya imani yako. Hivyo mtoto wa Mungu yeyote anapomwamini Kristo, na kuchukua hatua ya kumfuata YESU kweli kweli ni lazima apitie mahali hapo kujaribiwa kwa Imani yake kama kweli alimaanisha kuchukua uamuzi huo alijaribu tu?.

Hivyo mwanzoni tu unapoanza kumfuata YESU na kuachana na ulimwengu, vikwazo vinaibuka, pengine ndugu wataanza kukupiga vita, au kujitenga na wewe, pengine hali yako ya kiuchumi inaanza kuyumba, wakati mwingine unakosa chakula, na wengine wanakumbana na magonjwa, misiba, wengine wanafukuzwa kazi kutokana na Imani yao, wengine wanafungwa magerezeni, wengine wanaishia kupigwa, wengine wanadharauliwa, wanazushiwa majina mabaya, heshima yao inashuka kiasi kwamba mtu anaweza akafikiria yeye ni mtu wa bahati mbaya au ana mikosi, lakini si kweli, hapo ujue unajaribiwa kama utaiacha ile Imani au la.

Kumbuka hapa namzungumzia mtoto wa Mungu aliyeamua kumfuata BWANA YESU kwa moyo wake wote, na sio mtu yeyote tu ambaye hana habari na Kristo anapitia matatizo akidhani kuwa anajaribiwa, hapo ni shetani anafanya kazi juu ya maisha ya huyo mtu.

Lakini kwa wewe uliye amua kumfuata YESU kweli kweli, nakutia moyo usikatishwe tamaa wala usione ya kuwa una bahati mbaya au una mkosi, yakupasa usonge mbele kwani ni kitambo kidogo tu unatapitia hali hiyo baada ya hapo Bwana atakutengeneza na kukuheshimisha zaidi.

1 Petro 5:9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.

[10]Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, MKIISHA KUTESWA KWA MUDA KIDOGO, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, NA KUWATIA NGUVU.”

Anasema tena..

1 Petro 4:12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ILI KUWAJARIBU, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.

[13]Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, FURAHINI; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.

[14]Mkilaumiwa KWA AJILI YA JINA LA KRISTO NI HERI YENU; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.

[15]Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.

[16] LAKINI IKIWA KWA SABABU NI MKRISTO asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.

Je umemfuata Yesu kweli kweli?? Onyesha chapa za Yesu?, onyesha ni wapi ulipitia changamoto kwasababu ya Imani yako? Ni wapi ulidharauliwa, au ulichekwa, au ulitengwa, au uliaibishwa, au ulipigwa, au ulitukanwa, au uliteseka, au ulishushwa chini n.k, kwa ajili ya kuchukua uamuzi wa kumfuata Kristo?? Kama bado basi ujue bado hujaanza safari ya kumfuata yeye. Bado upo Misri haijalishi unaenda kanisani namna gani, unaimba kwaya kiasi gani, unapaswa uchukue uamuzi wa moja kwa moja kumfuata YESU. Kuweka mawazo yako mbinguni, na kusema mimi duniani ni mpitaji makao yangu ni mbinguni , Mimi na dhambi basi!!

Bwana Yesu akubariki.

Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.”

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *