Sehemu ya kwanza 01 A.
Shalom nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu.
Karibu katika sehemu ya kwanza hii fatilia somo hili ni muhimu sana litakusaidia kupitia somo hili ukawe mwanzo wako mpya wa kuishi katika ukweli huu.
Kuna mafundisho mengi yasiyokua sahihi katika mwili wa Kristo na yamekubalika na kuwa na nafasi kubwa sana na kuonekana kana kwamba ni ya kweli na ni kwa sababu yana gusa maisha ya watu kwa sehemu kubwa basi yameonekana ni ya kweli na yakawa na nafasi kwenye maisha ya Watoto wa Mungu.
Awali ya yote ni vizuri kwanza kutambua saikolojia ya mwanadamu jinsi ilivyo na shetani siku zote ni dhaifu lakini huwa anacheza sana na saikolojia za Wakristo wengi na anajikuta anawadangaya kwa sehemu kubwa lakini uhalisia sio kweli.
Ni vizuri kujua akili ya mwanadamu inaamini kwa haraka jambo baya kuliko jambo zuri, yaani mtu akiota ndoto mbaya ni rahisi sana kuamka kuomba na kukemea na kuvunja sio vibaya kukemea ila mwanadamu huyo huyo akiota ndoto nzuri, yeye amekaa hata ana Kristo yupo mbingu mpya na nchi mpya ameshafika kule na kapewa taji ya haki ni ngumu sana kuchukua hata dakika 20 kuanza kumshukuru Mungu na kumtukuza kwa ajili ya ndoto hiyo na ya kwamba itimie kama ilivyo.
Au mtu akiambiwa na rafiki yake “nimeota uko stand uko uchi watu wanakushangaa sana nk au nimeota umekufa nk ni rahisi kuitafakari sana hiyo ndoto na kuanza kukemea lakini akiambiwa “nimeota uko na Bwana Yesu, ukihubihuri na watu wengi wanaokolewa kupitia wewe ” utasikia majibu “atukuzwe Bwana ” walakini ngumu hata kufunga na kuomba ili hilo jambo lifanikiwe nk”
Tafakari umeota ndoto ngapi nzuri na hujamshukuru Mungu? Ukachukulia kawaida hata usiombe Mungu jambo hilo liweze kupata nafasi ikiwa umeona watu wanaokolewa kupitia wewe unapo hubiri injili nk.
Si lengo langu kufundisha jambo hili ila ni mfano na katika huu utakua umejifunza na lengo langu ni kukuonyesha jinsi mwanadamu kwa sehemu ndogo tu alivyo na akili yake jinsi inaamini kwa haraka zaidi kuhusu jambo baya kuliko jambo zuri.
Watu wanaamiinishwa mambo ambayo si kweli, na watu wanatumia nguvu sana kushindana na kufunga lakini mwisho wa siku kunakuwa hakuna ushindi badala yake watu wanakaa katika eneo moja hilo hata uombaji wao unakuwa kama hauna matokeo.
Sasa tutaangalia jambo moja kwa siku ya leo kisha tutaendelea na sehemu ya pili.
- LAANA ZA UKOO, KUSHIKIRIWA NA VIFUNGO VYA KIFAMILIA NA JINSI YA KUJITOA
Haya ni moja ya mafundisho ambayo yanaaminika kuwa na nguvu kubwa sana na yanaaminika kuwa ni ya kweli na watu wengi sana wanatapeliwa na kukesha kuomba kutoka kwenye vifungo na laana za ukoo nk lakini ukweli ni kwamba sio fundisho sahihi na linalotakiwa kuchukua nafasi kubwa katika kanisa la Mungu.
(sisiemi kwamba vitu hivyo sio halisi ni halisi kabisa lakini sio kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili, maana kifo cha Yesu kilimaliza kila kitu).
Kwanini nasema hivi… “tunatumia hisia na kuona hivi vitu kweli vimetushika katika maisha yetu na tunaanza kulinganisha matukio na mambo tuna thibitisha kuwa ni kweli”
lakini hatuioni au kuielewa nguvu ya damu ya Yesu Kristo, hatuoni nguvu ya msalaba pale Kalvari.
Laiti kama tukielewa uweza, nguvu ya damu ya Yesu Kristo na kujua nini imefanya kwa ajili yetu basi hatuwezi kuona hizi laana za kiukoo na za kifamilia na kujitoa kwenye vifungo vya kipepo vikipata nafasi ndani yetu.
Ikiwa Yesu Kristo amekutoa katika ufalme wa giza na kukuleta nuruni amekutoa katika vifungo na katika utumwa wa kila namna na ukawekwa kuwa huru inawezekana vipi ukawa tena kwenye vifungo mpaka uanze kujinasua tena wewe kwa maombi mengi?
maana yake ni dhahiri hujaielewa kazi ya Yesu pale msalabani.
Naomba utafakari hili andiko hapa na liamini andiko usiamini hali unazoziona, usiamini hisia zako zinavyokutuma hebu liamini Neno hili…
Waebarania 2:14-15 “[14] Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,
[15] awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.”
Sisi tumeshiriki mwili na damu yake maandiko yanasema yeye alishiriki hayo ili kwa njia ya mauti yake yeye aliyekua na nguvu za mauti yaani ibilisi amharibu.
Kumbe adui tayari ameshaharibiwa na Bwana Yesu na hana nguvu juu yetu sisi sasa kwa nini tunamuona kuwa ni tishio na Bado katufunga?
Angalia mstari huo wa 15 anasema nini? Anasema awaache huru ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikua katika hali ya utumwa maana yake sisi ambao tulikua katika hali ya utumwa tumewekwa huru na tumeondolewa katika utumwa. Sasa kwa nini uendelee kukaa na kujiona uko utumwani? Je nguvu ya Yesu ni ndogo?
Jibu ni hapana, ufahamu wako ndio umekua mdogo kuelewa na kuamini kile ambacho Kristo amekifanya kwa kifo chake msalabani.
Wakristo wengi wana mwambudu Mungu kwa hofu hawana uhakika na wokovu wao kwa sababu ya kutokujua nini Kristo alifanya katika maisha yetu sisi.
Luka 1:74 “Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,”
Kama laana zinafanya kazi kwa mwamini basi tungeona Paulo akiomba maombi hayo, petro akiomba maombi hayo.
Lakini hatuoni wakiomba maombi hayo kwa sababu walimuelewa Kristo na walijikita na kuwafundisha watu wamuelewe Yesu Kristo katika maisha yao na wakimuelewa basi watakua huru kweli kweli usiwe mtumwa wa fikra za kishetani na kuamini mafundisho ambayo hayana msingi wowote wa kimaandiko.
“Utumwa wa mwamini unaanzia katika fikra”
Wengine mpaka wanaambiwa dhambi ambazo baba zao au ndugu zao bado zinawafata na wako katika wokovu wanapaswa kutubu, wanapaswa kutoa sadaka huo sio ukweli ni uongo maandiko yanasema nini?
Wakolosai 1:13 “ Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
14 ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;
15 naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”
Maandiko kwenye mstari wa 14 yanasema katika yeye tuna ukombozi yaani msamaha wa dhambi sasa tunapoongelea msamaha wa dhambi hatuongelei dhambi hizi unasema wizi, uzinzi hizi ni moja wapo lakini msamha wa dhambi ni inajumuisha kila kitu ikiwemo laana nk na ndio maana maandiko yanasema…
Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;”
Laana zote Kristo alichukua juu ya mtu na ndio maana akasema “ IMEKWISHA ” Kristo hakubakisha kitu kingine chochote.
Anza kubadilisha ufahamu wako leo ndipo utaanza kuona ukweli na uhuru halisia ndani ya Yesu Kristo.
Ubarikiwe sana tutaendelea na sehemu ya KWANZA 01 B
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255613079530 au +255693036618
Bwana akubariki.