
TULICHAGULIWA TANGU AWALI
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze Maneno ya Mungu, kwa Neema zake, leo tutajifunza somo linalosema, Kuchaguliwa kabla ya kuwekwa misingi ya Ulimwengu.
Waefeso 1:5-14 “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe KWA NJIA YA YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.
[6]Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.
[7]Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.
[8]Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;
[9]akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo.
[10]Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo;
[11]na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, HUKU TUKICHAGULIWA TANGU AWALI sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.
[12]Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
[13]Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.
[14]Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.”
Je! umechaguliwa tangu awali?? Utajuaje kuwa ulichaguliwa??
Kwa kuwa mtakatifu kama yeye alivyo, kwasababu anasema ametuchagua tuwe watakatifu.
Waefeso 1:4 “kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ILI TUWE WATAKATIFU, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
Utakatifu ndio utambulisho wa kuwa ulichaguliwa au la, na utakatifu ni wa mwilini na rohoni wala hakuna nusu nusu.
Maana halisi ya utakatifu sio kutokuwa na makosa kabisa, bali ni kuwa na mabadiliko kila siku kuelekea ukamilifu. Sasa jiulize tangu ulivyohubiriwa kuwa kuvaa suruali kwa mwanamke, kuvaa vimini, nguo za kubana, kupamba mwili kwa hereni, mekaps, lipsticks, kusuka, kubadili rangi za kucha ni machukizo kwa Mungu je umebadilika??
Tangu ulivyoshudiwa kuwa kutazama picha za ngono, kucheza magemu, kubeti, kushabikia mipira, miziki na kufuatilia filamu zenye maudhui ya kidunia ni kujichafua nafsi yako na kujitenga na Mungu je uligeuka na kiviacha hivyo vitu??.
Ni mara ngapi ulihubiriwa uache kunyoa mitindo ya kidunia/denge, uache makundi mabaya, uache kujichua, uache kujisaga, uache madawa ya kulevya, uache uasherati, uache pombe, uache kiburi, chuki, usengenyaji, uongo, kutokusamehe na mambo yote mabaya na hutaki kuacha!!!
Jiangalie leo unasikia sauti ya Roho Mtakatifu anakushudia moyoni mwako je upo tayari kutii na kubadilika?? Ukiwa tayari leo basi utakuwa miongoni mwa wateule wa Mungu waliokusudiwa uzima wa milele. Lakini ukiendelea na maisha yako ni wazi kuwa upo miongoni mwa wale waliowekwa hapa duniani kutimiza kusudi fulani la Mungu na baada ya hapo kwenda kuharibiwa.
Mithali 16:4 BWANA amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.
Sasa utajiuliza kwanini Mungu mwenye upendo afanye hivyo, awafanye watu wengine kwa ajili ya mabaya, jibu rahisi ni kwamba..
“..ni nani ashindanaye na kusudi lake?
[20]La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
[21]Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?
[22]Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;
[23]tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;”(Warumi 9:21-23).
Matendo ya Mitume 13:48 Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.
Natumai u miongoni mwa waliokusudiwa uzima wa milele.
Bwana Yesu akubariki kwa baraka zote za rohoni na mwilini.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.