
SHARTI HUU UHARIBIKAO UVAE KUTOKUHARIBIKA.
Shalom mtu wa Mungu, karibu tuzidi kujifunza maarifa ya ki-Mungu maadamu ile siku inakaribia.
Neno la Mungu linatufundisha kuwa kuna siku tutavikwa miili ya utukufu yenye hadhi ya kimbinguni, miili isiyo na udhaifu, isiyougua wala kufa.
Katika siku hiyo, parapanda ya Mungu italia, na wote tuliomwamini Yesu, tulio hai..kama hatutakufa mpaka siku ile ya kurudi kwake, basi tutamwona Bwana akitokea mawinguni, na kisha wafu waliopo makaburini nao pia wataisikia sauti ya parapanda, na wao pia watafufuka.
Katika siku hiyo, kama mtu alikufa katika udhaifu fulani labda alikufa akiwa kiwete, au kiziwi au kipofu, au alikufa na ugonjwa wa kansa, lakini alikuwa ndani ya Imani, basi atafufuliwa na kurudi katika mwili wake, akiwa mzima kabisa, akiwa si kipofu tena, wala si kiziwi tena, wala si kiwete tena, wala si mgonjwa tena, kama mtu alikufa na Kisukari, basi atafufuliwa bila huo ugonjwa.
1 Wakorintho 15:40 “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.”
Katika siku hiyo baada ya ufufuo, tukiisha fufuka na kuwa na miili yetu ya asili isiyo na kasoro hata moja…kufumba na kufumbua tutabadilishwa miili yetu hii na kuwa miili ya utukufu..pamoja na wale watakatifu ambao watakuwa hai watabadilishwa pia. Kumbuka hatutavuliwa hii ya asili ambayo imeshafufuliwa…hapana…bali ni hii hii itabadilishwa na kuwa ya kimbinguni.
Au vinginevyo ufufuo utakuwa hauna maana…Kwasababu huko huko tulipokuwepo tungepewa hiyo miili ya utukufu…lakini unaona lazima tufufuke kwanza kama Bwana Yesu alivyofufuka..turudi kwenye miili yetu ya asili kisha miili hiyo ibadilishwe.
1Wakorintho 15.51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.
53 MAANA SHARTI HUU UHARIBIKAO UVAE KUTOKUHARIBIKA, NAO HUU WA KUFA UVAE KUTOKUFA.
54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda”
Unaona?..Hii inayokufa itavaa kutokufa..sio kwamba itatoweshwa na kuletwa mingine..hapana ni hii hii.
Sasa miili hiyo itakuwa imevikwa uwezo wa ajabu wa kimbinguni… …Uwezo huo ndio kama ule wa Bwana Yesu aliokuwa nao baada ya kufufuka na ule malaika watakatifu walionao sasa.
Unakuwa unauwezo wa kula na kunywa lakini hauishi kwa kula wala kunywa, Bwana Yesu alipofufuka alikula samaki na wanafunzi wake akatoweka na chakula kile tumboni mwake lakini hakuishi kwa hivyo na hata sasa haishi kwa hivyo…Na pia mwili huo unakuwa na uwezo wa kubadilika badilika kama Malaika. Bwana Yesu baada ya kufufuka sehemu nyingine alionekana na sura nyingine(Marko 16:12)..sehemu nyingine alionekana kama malaika..(Yohana alimwona kwenye maono akiwa na macho kama miale ya moto), mwenye mavazi yanayong’aa sana.. Hata leo hii Bwana anaweza kumtokea mtu kwa umbo la mwanadamu wa kawaida kabisa akakaa naye na kula naye..na anaweza pia kumtokea mtu kwa umbo kama la malaika mwenye utukufu mwingi na mwanga mkali hata mtu asiweze kumtokea..kama alivyomtokea Mtume Paulo. Hizo zote ni tabia za huo mwili mpya wa utukufu. Na sisi tutakapofufuliwa tutafanana na Bwana Yesu katika kila engo..miili yetu itakuwa na tabia hizo hizo.
Mwili huo pia una uwezo wa kupotea na kutokea mahali pengine kama Bwana Yesu, na pia una uwezo wa kupaa bila mbawa kama Bwana Yesu alivyopaa mbinguni ndio maana siku ile ya unyakuo tutapaa mbinguni na wengine hawataweza, na una upeo mkubwa wa kujua mambo yote. Na tabia nyingine nyingi, za kimbinguni mwili huo unao…ambazo hatuwezi kuzijua zote mpaka tutakapovikwa miili hiyo.
Hivyo itakuwa na uchungu sana kukosa kuvikwa mwili huo..Itakuwa ni uchungu sana wakati wa unyakuo wakati watakatifu wengine wanafufuliwa sisi tuwe tumebaki mautini. Ni heri tuteseke sasa lakini siku ile hatutateseka…ni heri tuonekane tumepoteza kila kitu hapa lakini mbele za Mungu tuonekane hatujapoteza kitu.
2Wakorintho 5:1 “Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.
2 Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni;
3 ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi.
4 Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twaugua, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima”.
Ni heri uonekane mjinga na mshamba leo kwa kutokuvaa vimini, na masuruali, na kutokuweka makeup, ni heri ukafukuzwa kazi leo kwa kukataa kufanya uasherati, ni heri ukapitia kila aina ya dhiki leo kwa ajili ya Kristo hata ikiwezekana kufa…Lakini Bwana wetu Yesu alisema maneno haya..
Luka 21:17 “Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu.
18 Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu.
19 Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”.
Tunaishi katika nyakati za mabadiliko hayo, siku yoyote parapanda italia na wafu waliokufa katika Bwana Yesu, watafufuliwa na kurudia miili yao ya asili kisha wataungana na watakatifu walio hai na kwa pamoja wanavikwa miili hiyo ya utukufu na kisha tutanyakuliwa juu mbinguni kumlaki MFALME YESU Bwana wetu.
Siku hiyo kutakuwa na furaha na shangwe kuu sana, kwa mara ya kwanza tutaacha hii ardhi na kupaaa juu sana..tutapokelewa na maelfu ya malaika wa Mungu, tukiwa wageni kwa mara ya kwanza tunaingia mahali Mungu aliko, tunaona mambo ambayo jicho halijawahi kuona, tutashangaa sana mambo mengi yasiyoisha maajabu yake, hakika itakuwa ni furaha tele, wakati huo tutakuwa tumesahau taabu zote tulizowahi kupitia hapa duniani, hatutakumbuka tena kama tumewahi kupitia dhiki kwasababu ya furaha kubwa tutakayokuonayo, tutakaribishwa katika karamu ambayo Bwana alituandalia wageni wake kwa miaka mingi, tutakula na kunywa mezani pa Bwana, tutawaona ndugu zetu waliofia Imani wakina Paulo, wakina Stefano, na manabii wote kuanzia Ibrahimu, na pia tutamuona baba yetu wa kwanza Adamu, tutamuona Enoko kipenzi cha Mungu, tutawaona wakina Nuhu, tutawaona dada zetu na mama zetu wakina Hawa, Sara, Rebeka, Mariam, na wengine wengi, tutasalimiana na kuulizana maswali mengi, hakika itakuwa ni siku ambayo haijawahi kutokea na haitatokea tena, katika siku hiyo hili neno litatimia..
Isaya 25:6-9 “Na katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.
[7]Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.
[8]Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo.
[9]Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.
Swali la kujiuliza kwa wewe uliye nje ya wokovu, au uliye vuguvugu, siku hiyo utakuwa wapi wakati watakatifu wanafufuliwa na kuvikwa kutokuharibika??. Kwasababu watakaoshinda mauti si wote!, bali ni wale waliokufa katika Kristo tu!, walioyatakasa maisha yao walivyokuwa duniani.
Kama hujaokoka..Ni vizuri ukafanya hivyo leo, usingoje Kesho kwasababu biblia inasema “hujui yatakayozaliwa ndani ya siku moja”..Kifo ni kama usingizi..hujui saa utakayopotelea usingizini. Hivyo tubu sasahivi hapo ulipo…Jitenge dakika chache jitenge peke yako.Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia.. ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
Ee mungu baba, naja mbele zako, nikiwa ninajitambua kuwa mimi ni mkosaji na nimekutenda dhambi nyingi, na kwamba nimestahili hukumu. lakini wewe Mungu wangu ulisema katika neno lako kuwa wewe ni Mungu wa rehema unayewarehemu maelfu elfu ya watu wanaokupenda wewe. na leo hii ninakuja mbele zako nahitaji msamaha wako na msaada wako Mungu wangu, ninatubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha na kwa moyo wangu wote, .
Ninakiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana, na yeye ndiye mwokozi wa huu ulimwenguni. hivyo naomba damu ya mwanao takatifu inisafishe uovu wangu wote sasa nifanyike kuwa kiumbe kipya kuanzia leo na hata milele.
Asante Bwana Yesu kwa kunipokea na kunisamehe.
Amen”.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Ulikuwa na miziki ya kidunia kwenye simu yako ifute yote sasahivi usiache hata moja, kulikuwa na watu unamahusiano nao ya kiasherati, futa namba zao sasahivi.
Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo namna hiyo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Na kuna Amani fulani itaingia ndani yako ambayo hiyo ndio itakuwa uthibitisho wa wawe kufanyika kiumbe kipya. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Bwana akubariki sana.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.