
WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA
2 Wakorintho 6:1-2 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
2](Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
Mungu alipotengeza hii dunia, aliweka kila kitu katika wakati wake, ndio maana kuna wakati wa usiku na wakati wa mchana, pia kuna wakati kiangazi na wakati wa masika, kuna wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa, kila kitu kipo katika wakati wake, hebu jaribu kuchunguza utaliona hilo.
Mhubiri 3:1-8,11 “Kwa KILA JAMBO kuna majira yake, Na wakati kwa KILA KUSUDI chini ya mbingu.
[2]Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa;
[3]Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
[4]Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;
[5]Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
[6]Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;
[7]Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;
[8]Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.
[11] KILA KITU amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.
Umeona, kila kitu kina wakati wake, hata wakovu una wakati wake, lakini kwa bahati mbaya si kila mtu anafahamu wakati wake anaoishi na nini anapaswa kufanya kwa wakati huu..
Yeremia 8:7 Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za BWANA.
Koikoi, mbayuwayu na korongo ni ndege wa ajabu sana, ni ndege wenye uwezo wa kusoma majira ya dunia, Na hiyo imewasaidia sana, kuishi maisha ya salama salmini huku duniani, pasipo kukumbana na changamoto zozote zisizo na maana
Hawa ni ndege ambao kikikaribia kipindi cha baridi wanahama wote maeneo yao wanayoishi kwa muda, na kusafiri umbali mrefu sana, kwenye pembe ya pili ya dunia kutafuta msimu tulivu aidha wa vuli au wa joto ulipo wakatulie, kisha baadaye hali ya baridi ikishakwisha wanarudi katika makazi yao ya awali kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Ndege hawa, wanaelewa kabisa kwa namna ya kawaida hawawezi kuishi katika mazingira hayo ya baridi kali, kwasababu hata viota vyao vitaganda.. Sasa ili kulitatua hilo tatizo inawagharimu wahame kwa muda, ndio hapo wanasafiri maelfu ya kilometa wanakuja mpaka huku kwetu Afrika, au nchi nyingine zenye joto, wanakaa huko mpaka msimu wa baridi utakapokwisha kule Ulaya ndio wanarudi sasa, kuendeleza maisha yao ya sikuzote.
Ndege hawa wasio na akili kama sisi, wanajua majira na nyakati za kujiweka salama, lakini sisi tunashindwa kujua wakati wa neema ni upi, na wakati wa hukumu za Mungu ni upi.. Sisi tupo tu hatujui majira yetu, tunadhani wakati wote, hii neema ya wokovu itaendelea kuwepo, tunadhani wakati wote, hali itakuwa kama ilivyo sasa hivi, utahubiriwa injili kama unavyohubiriwa sasa hivi..
Luka 19:41 Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,
[42]akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.
[43]Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;
[44]watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, KWA SABABU HUKUTAMBUA MAJIRA YA KUJILIWA KWAKO.
Ndugu yangu, fahamu kuwa neema hii inakwenda kuisha siku sio nyingi, Dhiki kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu dunia iumbwe na wala haitakaa iwepo itakwenda kutokea ulimwenguni kote..Dalili zote zinaonyesha, pengine katika wakati wetu huu tunaoishi tutayashuhudia hayo..Haya majira ya neema ndio yanaishia hivyo, muda huu tulionao ni wa nyongeza tu, dunia ingepaswa iwe imeshakwisha tangu zamani, lakini kwasababu tu ile nuru ndogo ya jioni ipo ndio maana unaona mambo bado yapo hivi..
Tupo katika mwaka wa Bwana, mwaka wa maachilio, wakati wa majira ya neema, wakati ambao mtu akiamua kuokoka kweli kweli anakubaliwa, kwasababu wakati uliokubalika ndio sasa. Kuna wakati ambao hautakubalika tena, wakati huo neema ya wokovu imekwisha ondoka… baada ya unyakuo wa watakatifu, na halikadhalika wakati usiokubalika ni pale mtu anapoiaga hii dunia, kule aendako hakuna nafasi nyingine hata kama ataenda kutubu kwa machozi mengi, huko hukana matumaini ya kuokolewa, ni kukaa katika giza nene huku ukiwa na majuto makuu sana.
Hivyo wakati wa kuokoka ni leo, ni muda huu unaposoma huu ujumbe, ukimaliza anza safari ya wokovu kwa kumaanisha kuacha dhambi zote unazozijua, unazozifanya kwa siri au kwa wazi, unaacha na namna zote za udunia unaenda kutafuta kanisa la kweli, unaenda kubatizwa kwa usahihi, unaanza safari ya imani kwa kujifunza biblia na kuukulia wokovu.
Kumbuka wakati uliokubalika ni sasa, usisubiri kesho au baadaye, ni sasa unapofikiwa na injili hii mahali popote ulipo, usisubiri mpaka utoke kazini uende nyumbani, hapo hapo kazini tafuta mahali pa utulivu na ungama dhambi zako kwa Mungu huku ukiwa unamaanisha kabisa kuziacha zote, maana yake ulikuwa umepamba mwili wako kwa mapambo ya kila namna, ondoa mapambo hayo, kama ni hereni ondoa, kama ni kucha bandia ondoa, au umepaka rangi futa, au kama umesuka fumua nywele zako kama huwezi mwenyewe tafuta mtu akusaidie, ulikuwa unavaa suruali, vimini, nguo za kubana tafuta namna yoyote uondoe na kuzichoma…omba hata ruhusa huko kazini ukabalishe na kuvaa nguo za heshima zenye utukufu kwa Mungu,
Ondoa na zingine ulizohifadhi kabatini..kagua nguo zote, tenga zile ambazo hazina utukufu kwa Mungu.. tafuta mafuta taa na kibiriti choma zote wala usiangalie gharama ulizonunulia, kumbuka unafanya hivyo kuinusuru roho yako na jehanamu, saficha na simu yako… futa miziki yote za kidunia na filamu zenye maudhui ya kidunia, futa magemu yote na michezo ya kamari, futa picha zote zinazokufanya uwe mtumwa wa zinaa, futa makala yote ya zinaa, left makundi yote yasiyo na maana, futa namba zote za watu uliokuwa unazini nao mpaka na wale mlio ahidiana kuoana futa waambie umeokoka na wao wanapaswa waokoke, rudisha mali zote ulizodhulumu, waombe watu wote msamaha ambao hampatani, kumbuka wakati uliokubalika ni sasa, hivyo hii toba ni sasahivi unapaswa kuanza kutubu, usiseme tayari umeokoka ingali hujawahi kutubu toba ya kweli, toba ya kweli ndio huu!! Na mtu yoyote ambaye hajatubu na kuacha hivyo vitu na vingine vinavyofanana na hivyo, mtu huyu kulingana na biblia hajaokoka!! Hata kama anahudhuriaga kanisani kila week, hata kama anajulikana kama mtumishi, mchungaji, askofu, mwanakawaya, n.k, hata kama ananena lugha za malaika maadamu tu hajaacha dhambi na ulimwengu huyo hajaokoka na kama ni wewe unayesoma ujumbe huu, basi ujumbe huu Mungu amekusudia kwako, fanya maamuzi sasa ya kuokoka.
Wakati uliokubalika ni sasa, usisubiri mpaka ushuke shimoni maana baada ya kuaga dunia hakuna nafasi nyingine!! Haijalishi utaenda kutubu kwa machozi mengi, wapo wengi wanatubu lakini huko hakuna matumaini, hakuna kusikiwa ni majuto makuu sana ndani ya giza nene, halikadhalika parapanda imekaribia sana, baada ya watakatifu kunyakuliwa hakuna tena kutubu na kuokoka, kusubiria tu dhiki kuu na ziwa la moto.
Wakati uliokubalika ni sasa, saa ya wokovu ni leo. Okoka leo kweli kweli!!
Maran atha. (Bwana anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.