JIBU
1,Wokovu
Hakuna namna utamshinda shetani ukiwa nje ya wokovu, kwasababu hata Wana wa Skewa hawakuweza kutoa pepo kwa jina la Yesu kwa sababu hata hao pepo waliwambia Yesu wanamjua na Paulo ,je ninyi ni akina nani?
Matendo 19:13 Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.
14 Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo.
15 Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? 16 Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.
Wokovu ni kukubali Kristo akae ndani yako, mtu anayekaa na Kristo humshinda shetani kwa sababu adui ajapo huona nguvu ya Kristo na hivyo mipango yote ya adui hushindwa.
2, Maombi, huaribu mipango yake shetani
Hii ni njia mojawapo ya kuharibu mipango ya shetani, mtu anaweza kuwa ameokoka lakini bado shetani akamletea majaribu kwa sababu hajasimama vizuri katika maombi,
Yesu alisema:
Mathayo 26:41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.
Yesu alikuwa mkamilifu hakuwa na dhambi kabsa lakini bado shetani alimjaribu, wewe je itakuwaje upande wako? Ukiwa mvivu wa kuomba, huwezi kuhudhuria mikesha utakuwa unampa nafasi shetani akuweke majaribuni. Unaweza kuona mambo yote yapo sawa lakini tambua tu ipo sehemu ambayo adui anakuharibia utaligundua hilo badae sana utakapoacha uvivu wa kuomba.
Wokovu huambatana na maombi, mtu anayeomba huzungukwa na moto mkali ambao shetani akiuona hawezi kufanya jambo lolote kwa mtu huyo.
3, Kubali kuwa mjinga
Kwa kufanya hivyo utamshusha shetani chini,
Warumi 16:19 Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.
20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]
Neno linatutaka tuwe wajinga katika mambo mabaya hii inatupa nafasi kubwa kwa Mungu na kumweka shetani mbali na sisi..
Kwa mfano, tunapokubali kupitwa na mitindo mipya ya kidunia, hatusikilizi miziki wala kuangalia muvi zinazotoka, yaani hatupotezi muda katika mambo ya dunia na badala yake tukatafuta ujuzi na hekima ya Mungu basi tutamshinda shetani kwa sababu hatuna chochote kilicho miliki yake. Tunapoipenda dunia tunakuwa na urafiki na shetani na kisha tunatengeneza uadui na Mungu.
4. Weka Neno la Mungu ndani yako,utamfukuza shetani
Inakupasa kufahamu ukweli wa kila neno unaloweka moyoni mwako, hii haimaanishi ukariri vifungu vya biblia, hapana. Yesu alipojaribiwa na shetani pale jangwani alimwambia kweli yote ya neno inavyosema..
Mathayo 4:6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.
Utaifahamu kweli ya neno la Mungu kwa njia ya mafundisho fasaha kutoka kwa waalimu maana hapo ndipo Roho Mtakatifu atakufundisha kupitia wao. Hata Roho Mtakatifu anaweza kukufundisha moja kwa moja ikiwa utampa nafasi ili usipotoshwe na adui kwa njia ya manabii wa uongo waliopo sasa hivi…
5, Utii wa neno, utastahimili majaribu yote ya shetani
Unapolifahamu neno na kujua kweli yote ya maandiko basi yakupasa kulitii neno ili usimpe shetani nafasi ya kukunasa katika mitego yake. Uwe mtendaji wa neno mara unapolisikia, ishi maisha ya utakatifu,
Yesu alisema kuna watu hulisikia neno na wasifanye chochote na wengine hilisikia neno na kulitendea kazi na wote hujaribiwa na mvua na mafuriko ya adui sasa yule aliyesikia tu neno bila kulifanyia kazi mafuriko ya adui humchukua. .
Mathayo 7:26 Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;
27 mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.
Kuna mambo mabaya huwapata watu kwa sababu ya dhambi, unapoishi maisha mtakatifu unamnyima shetani nafasi ya kukushambulia. Ishi kama neno litakavyo.
6, hubiri Neno, utamshusha adui kutoka juu
Watu wengi hawapendi kushuhudia wengine habari za Mungu. Tunapoitangaza habari ya wokovu adui hawezi kukaa juu ya anga hili kutupinga. Kuna wakati Bwana Yesu aliwatuma wanafunzi wake kuhubiri injili, nao walirudi kwa furaha na kumwambia Bwana hata mapepo yanatutii. Yesu aliwambia nalimwona shetani akianguka kutoka juu kama umeme. Hii ilionyesha kuwa kitendo cha wao kuhubiri injili kulimfanya shetani anguuke kwa kasi kubwa sana.
Mathayo 10:17 Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. 18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.
Utakapozingatia hayo mambo sita utakuwa umemdhibiti shetani kila mahali lakini pia utamteka. Ni wajibu wetu kurekebisha mahali ambapo hatujakaa sawa ili kwa umoja wetu tuujenge ufalme wa Mungu na kumshinda shetani..
Yakobo 4:7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.
Bwana akubariki
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.