MAISHA JE! SI ZAIDI YA CHAKULA, 

Biblia kwa kina No Comments

MAISHA JE! SI ZAIDI YA CHAKULA, 

Mathayo 6:25 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

Watu wengi tumepokea elimu fulani ya kudhani kuwa maisha ni kupata mafanikio ya mwilini kama chakula, mavazi, nyumba, pesa n.k, hivyo watu wengi wamekuwa wakihangaika huku na huku kutafuta hayo maisha…hata wengine wametumia njia sisizo halali ili wapate tu haya maisha.

Sio maisha mabaya, ni maisha mazuri kweli, kula na kunywa vizuri, kuvaa vizuri, kutafuta fedha na kuwekeza, kuwa na nyumba nzuri, kuwa na mke/mume bora, kuwa na watoto, kwa ujumla kuwa na mafanikio ya mwilini. Ni mapenzi ya Mungu tufanikiwe pia katika hayo.

3 Yohana 1:2 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.”

Lakini, Bwana Yesu alisema tusisumbukie hayo, kwasababu maisha ni zaidi ya hayo, maana yake kuwa mafanikio hayo sio maisha halisi ambayo mtu akipata anajifunia kuwa amepata maisha, hayo sio maisha.

Maisha ni nini basi?

Maisha ni kutafuta na kupata ufalme wa Mungu! mtu aliyepata ufalme wa Mungu ndiye aliyepata maisha…hata kama hajafanikiwa sana katika dunia hii.

Mathayo 6:31-33 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?

[32]Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.

[33]Bali UTAFUTENI KWANZA UFALME WAKE, NA HAKI YAKE; na hayo yote mtazidishiwa”.

Sasa kutafuta ufalme wa Mungu haimaanishi tu kuokoka na kumpokea Yesu, ni zaidi ya hapo! Kutafuta ufalme wa Mungu maana yake ni kuwekeza mawazo yako katika maswala ya kiroho, kutafuta kufanya mapenzi ya Mungu, kuyawaza sana, kutafiti na kujua sana elimu ya ufalme wa Mungu huko ndiko kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na hayo ndio maisha haswa. Bwana Yesu alisema tena..

Mathayo 13:52 Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye ELIMU YA UFALME WA MBINGUNI amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.

Sasa mtu huyu mwenye elimu hii ya ufalme wa mbinguni ndiyo ambaye amepata maisha, lakini hii elimu haiji tu yenyewe yenyewe kimiujiza bali inatafutwa kama vile ilivyo elimu ya dunia hii. Kuna kujitoa, na kupambana sana na kutumia muda mwingi na hata gharama kubwa kuupata. Kwahiyo hatupati tu kirahisi rahisi kwa kupokea Yesu na kwenda kanisani basi, hapana ni lazima tuweke bidii kutafuta, ndio maana alisema tena sehemu nyingine…

Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”.

Umeona hapo, inahitaji kutumia nguvu, yaani nguvu za kimwili na kiroho kuupata. Unakuwa mtu wa kuomba sana na kufunga, unasoma biblia na kujifunza kwa kina, unasoma makala nyingi za kiroho, unauliza kwa watu waliokutangulia kiroho, unajitoa kwa hali zote kufanya mapenzi ya Mungu, unatafuta tafuta sana kupata maarifa mengi ya kiMungu, ukiwa mtu wa namna hii kidogo kidogo utaanza kuuteka ufalme wa Mungu na hatimaye kuupata,…kwamaana kila atafutaye atapata.

Je! umepata ufalme wa Mungu? Au unatafuta kwanza maisha na kisha baadaye uje utafatute ufalme wa Mungu? Fahamu leo kuwa maisha halisi ni kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na hayo mengine Mungu atakuzidishia.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *