
MAKUTANO MENGI WALIPOKUWA WAKIFUATANA NAYE, ALIGEUKA AKAWAAMBIA..
Luka 14:25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,
[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.
Bwana wetu Yesu alipokuwa hapa duniani, huduma yake ilikuwa inakusanya watu wengi sana, na kwasababu alikuwa anafanya miujiza mingi sana kama kuponya magojwa sugu, kuwafungua waliopagawa na pepo, na hata kufufua wafu hivyo habari zake zilienea kote, watu walikuwa wanaambiana habari zake hivyo ni makutano mengi walikuwa wanamfuata.
Mathayo 4:23 Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
[24]Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.
[25]NA MAKUTANO MENGI WAKAMFUATA, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani.
Ni kama tu sasahivi, makutano mengi wanaokimbilia sehemu zenye miujiza ili watatuliwe haja zao, ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu, lakini yeye alipoona makutano mengi wanamfuata ili watatuliwe shida zao na huku hawana haja na Mungu..yeye aligeuka na kuwaambia..
“…Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”(Luka14:26)
Bwana Yesu hakuwa na lengo la kuwakusanya watu wengi kupitia miujiza yake, kwasababu nia yake sio kupata fedha kama manabii wa uongo wanavyofanya siku hizi. Lengo la Bwana ilikuwa ni kuwafanya watu wawe wanafunzi wake, na vigezo vya kuwa mwanafunzi wake ni hivyo alivyosema hapo juu KUACHA VYOTE.
Hebu leo wahubirie watu waache vyote wamfuate Yesu, yaani waondoe mali katika mioyo yao, wakubali kuacha ndugu zao na marafiki zao wanaowazuia wasimfuate Mungu, waache mionekano ya kidunia, waache kujipamba na kuvalia mavazi yasiyopasa jinsia zao, waache uasherati, waache pombe, waache kiburi, chuki, usengenyaji, rushwa, na mambo yote mabaya watasema unahukumu.
Maana hawapo tayari kuacha haya mambo na kumfuata Yesu na kuwa wakristo wa kweli, wao wanataka tu watabiriwe biashara zao ziongezeke, wanataka watatuliwe matatizo yao wakaendelee na maisha yao, wanafuata miujiza hawafuati Mungu…ndio maana wanakuwa wepesi kwenda kununua udongo, maji, mafuta, chimvi bila hata kufuatilia ukweli wa haya mambo yametoka wapi, wao wanachotaka ni mambo yao tu yaende vizuri basi.
Lakini maneno ya Bwana, ni yale yale hayajabadilika…kama mtu akitaka kumfuata na kuwa mwanafunzi wake hana budi kuacha vyote (anaposema kuacha vyote anamaanisha kuacha vyote vinavyozuia mtu kumfuata Mungu na kufanya mapenzi yake), hata kama yanapendeza macho au yanafurahisha nafsi kiasi gani unaikana nafsi yako unamfuata Yesu.
Hivyo ndugu unayesoma ujumbe huu, ni mapenzi ya Mungu ukutane na ujumbe huu mahali hapa, leo Yesu anakuambia acha vyote mfuate akufanye kuwa mwanafunzi wake, acha kuwa miongoni mwa makutano wanaofuata tu miujiza na kuponywa haja za miili yao na huku roho zao zikienda kupotea, fahamu kuwa muujiza mkubwa ambao unapaswa kutafuta ni muujiza wa kuacha dhambi na kuwa mwanafunzi wa Yesu, namaanisha kuacha ulevi, uzinzi, sigara, pombe, uchawi, hasira, uongo, uchungu, kutokusamehe, kutazama pornography, kujichua n.k, huo ndio muujiza namba moja, na hayo matatizo mengine yatasuluhishwa tu.
Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati na unyakuo umekaribia sana.
Maran atha(Bwana Yesu anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.