
NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI
Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maneno ya uzima.
Umewahi kusoma na kutafakari mara mbili mbili kauli hii aliyoisema Bwana Yesu muda mfupi kabla hajapaa kwenda mbinguni. Bwana Yesu aliwatokea wanafunzi wake ambao ndio sisi leo, akawaambia..
“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.
[19]Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
[20]na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Nataka tutafakari sana hilo neno ”NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI,” unajua unaweza ukawa unatembea na mtu kila siku lakini haujui mamlaka aliyonayo, lakini siku ukijua huwenda mtazamo wako utabadilika… pengine akikuambia mimi ni mkurugezi wa kampuni fulani, au mimi ni mkuu wa majeshi, mimi ni waziri au mfano akikuambia mimi ni mtoto wa raisi na nimepewa mamlaka yote kila mahali.
Bila shaka, ujasiri wako utaongezeka…hautaogopa ogopa tena kama ulikuwa unahofia kitu fulani. Kwasababu umeshajua mamlaka/nguvu ya mtu uliyenaye.
Halikadhalika katika ukristo, wengi wetu huwa hatumjui Yesu vizuri…tunamsomaga tu na kumsikia lakini hatujui nguvu alizonazo wala mamlaka yake. Siku tukijua hakika fahamu zetu zitabadilika kwa kiasi kikubwa.
Utakuta mtu amekaa ndani ya kanisa miaka kumi, ameokoka kweli lakini anaogopa wachawi, anaogopa hata kusikia majina yao.. mwingine anaogopa hata kutoka nje usiku, mwingine anaogopa wanadamu.. akitishiwa tu kidogo anaacha kuhubiri hapo, anaogopa kukamatwa, kupigwa n.k
Hajui kuwa huu ulimwengu sasahivi upo chini ya mamlaka ya Bwana Yesu, shetani ni kama mpangaji tu!..nyakati na majira yatakapotimia ataondolewa moja kwa moja, shetani sasahivi si kitu kwa Bwana Yesu..
Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, WALA HANA KITU KWANGU”.
Kwasababu gani, shetani hana kitu sasahivi kwa Bwana Yesu, kwasababu alishanganywa mamlaka yote pale Goligotha.
Wakolosai 2:15 “akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.
Enzi na mamlaka yaliyovuliwa hapo na Bwana sio yake yeye mwenyewe.. bali ni yale ya NGUVU ZA GIZA. Bwana amemvua shetani juu ya huu ulimwengu na wanadamu kwa kifo chake pale msalabani.. Na baada ya kumvua, akayavaa yeye mamlaka hayo.. (kumbuka mamlaka hayo ya shetani alimvua Adamu, pale Edeni).
Ndio maana alipofufuka katika wafu, aliwaambia wanafunzi wake waende kuhubiri injili kila mahali ulimwenguni kote bila kuogopa mtu yoyote..kwani aliyewatuma amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani, kwa maana nyingine kule mbinguni malaika wote akiwamo akina Mikaeli malaika mkuu wapo chini yake, huku duniani viongozi wote wa dunia…maraisi wote wapo chini ya mamlaka ya BWANA YESU, yeye sasa ndiye mkuu wa wafalme wa dunia (Ufunuo1:5), hakuna kitu kinaweza kufanyika bila yeye kujua na kupitisha. Hallelujah.
Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI”.
Hata sasa tunapozungumza Bwana Yesu anamiliki vitu vyote vya mbinguni na duniani, na vilivyopo chini ya dunia, na vitu vyote vinapiga goti, na vitapiga goti mbele zake.
Tukimwelewa Yesu kwa namna hii, kamwe hatakaa umwogope shetani, wala mchawi yoyote.. Ukiona unahofu ya shetani, au wachawi au watu Fulani na umesema umeokoka au umempokea Yesu, basi jua bado hujamjua Bwana Yesu vizuri.
Siku ukimjua na kumwelewa, hutabaki kama ulivyo.
Hivyo tafuta kumjua sana Bwana Yesu vizuri, zaidi ya kufuatilia nguvu za giza kwani hizo zote zipo chini ya mamlaka kuu (mamlaka ya Bwana Yesu mfalme wa wafalme)
Na kama hujampokea huyu YESU ipasavyo, fahamu kuwa Yesu ndiye mkuu wa uzima na ndiye njia ya kufika mbinguni. (Yohana 14:6), hivyo mgeukie leo kabla mlango wa neema haujafungwa maana tupo ukingoni sana.
Maran atha
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.