KAZI YAKO NI KAZI GANI?

Biblia kwa kina No Comments

KAZI YAKO NI KAZI GANI?

Shalom karibu tujifunze biblia.

Tukisoma ile habari ya Yona, kama wengi tunavyojua Yona alitumwa na Mungu kwenda kuhubiri katika mji ule wa Ninawi uliokuwa mji mkuu wa Taifa la ASHURU ambao ni maeneo ya Iran na Iraq kwa sasa.Lakini tunasoma habari haikuwa hivyo kwa nabii YONA, badala ya kwenda NINAWI mji wa ASHURU alioagizwa na Bwana, yeye akaamua kuubuni mji wake yeye alioupenda ili akakae huko, ndipo akakimbilia TARSHISHI mji uliokuwa nchi ya Lebanoni ili tu AJIEPUSHE NA MAPENZI YA MUNGU.

Lakini alisahau kuwa ili afikie malengo yake hana budi kupitia “NJIA YA BAHARI”.. Hivyo akaamua kupanda Merikebu zinazoelekea Tarshishi, Na kama tunavyosoma habari alipokuwa katikati ya safari yake bahari ilichafuka na mambo yakaanza kuharibika..wakati Yona akiwa ndani ya ile Merikebu amepumzika, watu waliokuwanayo walikuwa wakitaabika sana kwa hofu nyingi, ndipo baadaye wakapiga kura waone ni nani mwenye shida kati yao, na kama tunavyosoma, ile kura ikamwangukia Yona, Tunasoma…

Yona 1:1-10 “Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,

[2]Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.

[3]Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.

[4]Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.

[5]Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.

[6]Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.

[7]Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.

[8]Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; KAZI YAKO NI KAZI GANI? NAWE UMETOKA WAPI? NCHI YAKO NI NCHI IPI? NAWE U MTU WA KABILA GANI?

[9]Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.

[10]Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewajulisha”.

Sasa nachotaka tuone, ni hayo maswali aliyoulizwa Yona, na leo tutaangalia swali moja kati ya hayo, KAZI YAKO NI KAZI GANI?

Unaweza ukadhani, hayo maswali hayana maana sana, lakini nataka nikuambie yana maana sana na ndicho chanzo cha mafanikio au matatizo ya mtu.

Kazi anayoifanya mtu, inaweza ikawa chanzo cha kulaaniwa au kubarikiwa na Mungu, kuna kazi zingine ambazo mtu akizifanya moja kwa moja anakuwa chini ya laana, na ni lazima tu apatwe na matatizo ambayo hata yanaweza kupelekea mauti.

Kwa mfano kazi yoyote ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu, kazi isiyo halali, kazi inayomfanya mtu amkose muumba wake, kazi kama za kuuza madawa ya kulevya.. bangi, sigara, ugoro, n.k, au kuuza vilevi mfano pombe, au kilevi yoyote inayomfanya mtu aharibu mwili wake..hizo ni kazi ambayo mtu akifanya moja kwa moja anakuwa chini ya laana kwa kujua au kutokujua, na mkristo hapaswi kabisa kushiriki au hata kushikamana na kazi hizo haijalishi zinakipato kikubwa kiasi gani.

Vile vile kazi sisizo halali kama wizi, rushwa, utapeli, kubashiri/kubeti, ushirikina, ukahaba, kuuza mavazi ya ukahaba (suruali kwa wanawake, gauni za mipasuo, vitop, na mavazi yote yasiyompa Mungu utukufu), mavazi ya kihuni..

Kuuza vipodozi za kuchubua ngozi na kuuharibu uhalisia wa mtu, kazi ya kusuka nywele, kupaka kucha rangi, hivyo ni kazi haramu kwa mkristo na mtu anayezifanya yupo chini ya laana.

KAZI YAKO NI KAZI GANI?

Ni heri ufanye kazi inayokupa kipato kidogo lakini ni kazi iliyobarikiwa..kuliko kazi hizo zilizolaaniwa. Hivyo kabla hujakimbilia kuombewa kwasababu ya matatizo unayoyapitia sasa, hebu jiulize kazi yako ni kazi gani? Anzia kwanza hapo ndipo utafute vyanzo vingine vya matatizo yako.. maana huwenda kazi yako ndio chanzo cha ugonjwa wako, au hilo tatizo unalopitia.

Kumbuka hukumu ipo, na kila mtu atahukumiwa kwa kadri ya matendo yake, angalia kazi yako isije ikawa sababu ya kukupeleka jehanamu.

Je! umeokoka kweli kweli?? au umeokoka kwa namna ile ya kidini!!, Je! unafahamu kuwa unyakuo upo karibu sana na muda wowote parapanda italia na watakatifu kunyakuliwa.. jiulize utakuwa wapi wewe ikiwa ni leo usiku??

Bwana Yesu atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *