BALI, YEYE ASIYEJIZUIA NAFSI YAKE AMEKUFA INGAWA YU HAI.

Biblia kwa kina No Comments

BALI, YEYE ASIYEJIZUIA NAFSI YAKE AMEKUFA INGAWA YU HAI.

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe daima, Karibu tusikie injili ya Kristo iletayo wokovu wa roho zetu.

Neno la Mungu linasema katika..Timotheo 5:6 “Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai”.

Ikiwa kila kitu unakiruhusu kiingie ndani ya nafsi yako, kila kitu unakitamani, kila kitu unasikiliza, kila kitu unatazama, huwezi kujizuia, basi fahamu kuwa umekufa ingawa unaishi.

Ukitamani kuzini unaenda kutekeleza (kumbuka kuzini sio mpaka ulale na mtu..hata kuwaza tu tayari umezini), ukialikwa kwenye matamasha ya kidunia unaenda tu huwezi kujizuia, ukisikia kuvaa vimini na nguo za aibu unavaa, ukijisikia kutumia mkorogo unatumia, wewe ni sawa na mji usio na kuta!!

Mithali 25:28 “Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta”.

Ndugu yangu, kama upo katika kundi hili la wasiojizuia, basi amua leo kuokoka kweli kweli ili Bwana akupe Roho wake Mtakatifu ambaye atakusaidia kujizuia na mambo yote mabaya.

Biblia inasema moja ya dalili kubwa itakayotuonyesha kuwa tunaishi katika siku za mwisho ni kuwepo kwa wimbi kubwa la watu wasioweza KUJIZUIA. Na kutojizuia kunakozungumziwa hapo sio kujizuia kutokutokwa na haja, hapana bali kutojizuia kutenda maovu hadharani mbele za watu, hivyo si watu wema wanaozungumziwa hapa bali wanazungumziwa ni wale walio waovu, ili kutofautisha uovu ule wa nyuma na huu wa siku za mwisho, kumbuka waovu wa zamani walikuwa na kitu kinachoitwa Kujizuia, lakini waovu wa siku za mwisho biblia inaweka wazi kuwa hicho kitu hakitaonekana ndani yao kabisa.

2 Timotheo 3:1″Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

2 Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

3 wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, WASIOJIZUIA, wakali, wasiopenda mema,

4 wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

Ilikuwa zamani, mwanamke kahaba ni mtu wa kujificha, anafanya ukahaba wake kwa siri hata ni ngumu kumtambua, mavazi yake ya kikahaba alikuwa anayavaa usiku tu tena katika eneo la shughuli zake, nje ya hapo huwezi kumkuta, ilikuwa huwezi kumwona hadharani ovyo ovyo eti anazunguka na uwazi wake barabarani, haikuwahi kutokea hivyo wakati wowote. lakini angalia sasa, makahaba wanashindwa kujizuia kufanya mambo yao, wanakosa ule uwezo wa kutawala tamaa zao, ile hofu ya watu kuwaona na kuwachukulia hivi au vile haipo tena ndani yao, wapo tayari kupiga picha za uchi, na kutengeneza video zisizofaa ambazo hazistahili kabisa kuwepo, na kwa ujasiri kabisa wana zi-post katika mitandao, ili watu wote wawaone, na kibaya zaidi wanaofanya hivyo wengi wao ni watu wanaojulikana, ili kusudi kwamba uchafu wao uweze kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi, hizi ndizo ishara madhubuti za siku za mwisho.

Sio kana kwamba hayo mambo yalikuwa hayafanyiki zamani, hapana yalifanyika kwani biblia inatuambia hakuna jambo jipya chini ya mbingu, lakini kwanini unaona kama siku hizi maovu yameongezeka zaidi ya zamani,? Jibu ni kwamba hayajaongezeka kwa kiwango kile unachofikiri bali kinachoendelea sasa ni kwamba wafanyao maovu wa sasa wamepoteza kile kitu kinachoitwa kujizuia ndani yao..Roho ya kutokujali lolote imewavaa, roho ya “fuata mambo yako”, roho ya “ishi maisha yako”..roho ya “kutokujali” ndio inayotawala maisha yao. Na ndio maana hushangai hata kuona watu wa karne hizi watu waki-tengeneza video wanazini na wanyama n.k..Si ajabu tena kwao, kudhihirisha aibu zao wazi. Inasikitisha sana!

Kutukana hadharani hakukuwepo zamani, lakini sasa viwango vya matusi vimekithiri, mabarabarani, kwenye nyimbo za kidunia, kwenye mitandao, si watu wazima si watoto wadogo, maneno yanayozungumzwa huwezi kuamini kama marika kama hayo yanaweza kutoa maneno magumu kama hayo katika vinywa vyao.

Mashoga na wasagaji, wanajitangaza hadharani, hawajali tena hata vyombo vya dola na huku wanajua kabisa kwamba Sheria za nchi haziruhusu vitendo hivyo na kwamba mtu anayefanya hivyo adhabu yake ni kali, wao hilo wanaliona kabisa hawalijali sembuse Mungu wasiyemwona?. KUTOJIZUIA.

Ndugu yangu. Kama vile hilo andiko linavyosema “siku za mwisho kutakuwako na nyakati za HATARI ”. Fahamu kuwa nyakati zenyewe ndio hizi tunazoishi..Ikiwa utashindwa kujizuia mwenyewe na kuona kila kitu kufanya ni SAWA TU!…Zamani ulikuwa unaona aibu kuvaa vimini na kutembea navyo barabarani lakini sasa unaona hakuna shida yoyote! Ujue kuwa upo katika hatari kubwa sana..roho ya kutokujali imekuingia, na biblia inasema mtu wa namna hii AMEKUFA INGAWA YU HAI.

Ukiona zamani ulikuwa ukitukana unajisikia vibaya lakini sasa matusi yamekuwa ni sehemu ya maisha yako. Ujue kuwa ile roho ya kutokujali imekuvaa..Kama vile wale watu wa sodoma na gomora, jinsi walivyokuwa na tabia ya kutokujizuia hata kufikia hatua ya kutaka kulala na wageni wale (malaika wa Mungu) waliokuja yamkini kusitiri uovu wao, lakini wao wakashindwa kujizuia. Jambo gani lilitokea muda mfupi baada ya pale? Kwanza kabla hata maangamizi hayajawafikia walipigwa upofu. Na upofu ule ni wa daima..Vivyo hivyo na kwa watu wasiojizuia sasa, Upofu unakuja, na upofu huo ni wa daima, ukishamkuta tu mtu, basi huyo mtu hata afanyeje ni wa kuangamizwa tu! hawezi kutubu tena, neema inakuwa haipo tena juu yake, hata ahubiriweje injili, anakuwa tu kama mtu aliyekufa na kwenda kuzimu ingawa yeye anaishi duniani.

Tubu dhambi zako sasa, ukabatizwe upate ondoleo la dhambi zako kabla hujafa kabisa.

Maran atha (Bwana Yesu anarudi)

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *