IKIMBIENI ZINAA

Biblia kwa kina No Comments

IKIMBIENI ZINAA

Jina la Yesu Kristo mkuu wa uzima libarikiwe sana. Siku ya leo tutaenda kufahamu jinsi ya kushinda dhambi ya uzinzi na zinaa.

Dhambi ya uasherati na uzinzi ni dhambi inayoongoza kwa kuwapeleka wengi kuzimu. Lakini leo kwa msaada wa Roho Mtakatifu tutafahamu njia pekee ya kushinda dhambi hii.

Biblia inatufundisha njia ya kushinda dhambi hii ni KUKIMBIA TU, hiyo ndio njia ya kushinda!!. Hakuna njia nyingine ya mkato,

1Wakorintho 6:18 “IKIMBIENI ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.

Kumbuka anasema Ikimbieni!! Maana yake dhambi hii sio ya kuikaribia kabisa, ni kukanayo mbali mita nyingi sana.

Sasa tutaikimbiaje?

Kwanza tunaikimbia kwa KUOKOKA, yaani kwa kuzaliwa mara ya pili. Mtu ambaye hajaokoka (namaanisha wokovu wa kweli wa kuacha dhambi na kumpokea Yesu) hawezi kamwe kushinda zinaa haijalishi atajitahidi kujizuia kwa nguvu zake zote.

Ukishaokoka kabisa kabisa, hapo unapewa uwezo wa kukimbia dhambi hii..huo uwezo unapewa na Roho Mtakatifu atakayeingia ndani yako, anachokifanya Roho Mtakatifu ni kuua kiu ya kutamani tamani ovyo, anakupa uwezo wa kutawala mwili wako.

Lakini Roho Mtakatifu hafanyi kazi kama pepo ndani ya mtu, pepo akiwa ndani ya mtu anamuongoza yule mtu kutenda mambo ambayo hata yeye hataki, anamtumikisha, na wakati mwingine anamuondolea fahamu zake.

Lakini Roho Mtakatifu hafanyi hivyo, bali anakuwa kama msaidizi kwa mtu, anamuongoza kwa jinsi yule mtu anavyotamani kuongozwa naye..Roho Mtakatifu hamuondolei mtu ufahamu wake na kumpeleka peleka kama pepo, anatembea na mtu kama rafiki, anakushauri na anakupa sababu ya kutofanya hiki na kile, wakati mwingine anaweza kuugua ndani yako pale unapotaka kufanya jambo fulani lisilompendeza, sasa usipotaka kutii hiyo sauti yake wewe ukaendelea kuwaza unavyowaza, ukaendelea kung’ang’ania na kushikilia msimamo wako, basi Roho Mtakatifu anakuacha utimize mapenzi yako, kama ni picha chafu ulikuwa unatazama anakuacha uendelee kutazama, na mwisho wa siku shetani atakuangusha kwenye zinaa. Lakini mwanzoni wewe ulikubaliana na mahubiri ya shetani na tamaa ya moyo wako ukakataa kumtii Roho Mtakatifu alivyokuwa anaugua ndani yako.

Lakini ukimtii Roho Mtakatifu anakupa nguvu ya kushinda tamaa zote ambazo singekupeleka kuangukia katika dhambi ya zinaa, pale unapokutana na mazingira ambayo yangekunajisi Roho Mtakatifu anakusaidia kukuepusha na mazingira hayo, hata utakapoingiwa na mawazo ya uzinzi kutokana na vitu ulivyovitazama au kuvisikia bila kutarajia, Roho Mtakatifu anakusaidia kuondoa hizo kumbukukumhu ndani yako na unajikuta hayo mawazo hayakai ndani yako(anakusahaulisha), lakini hii inakuja kwa wewe kwanza kumtii.

Tunakimbiaje zinaa??

Unakaa mbali na vichocheo vyote vya zinaa kama hizo picha chafu, filamu zenye maudhui hayo, mazungumzo yenye maudhui hayo, kwa mfano huwezi kusema umekimbia zinaa na huku simu yako umejaza vichocheo hivyo, unasikiliza makala ya zinaa, unasoma na kufuatilia magroup zenye maudhui ya zinaa, unazungumza na kuchati chati na watu wa jinsia nyingine kila mara,

Yusufu alipotafutwa na yule mwanamke kwa matamanio yake…ilifika kipindi Yusufu hakutaka tena kuzungumza naye.

Mwanzo 39:10 Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini HAKUMSIKIA alale naye, WALA AONGEE NAYE.

Na biblia inasema mazungumzo mabaya huharibu tabia njema (1Wakoritho15:33), utasema ninaweza kujitawala, ni kweli mwanzoni utaweza lakini kidogo kidogo utajikuta tu umezama bila hata kujua ni muda gani umepitiwa, ni kama tu mtu anayelala na kupotelea kwenye uzingizi, hajui ni saa ngapi amepitiwa!! Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejaribu kusogelea mazungumzo mabaya au kuwa na ukaribu na mazungumzo hayo, na unajua shetani ni vigumu kutumia watu ambao hawako katika Imani kukuangusha, kwasababu hawezi kukupata kirahisi…anatumia mwamini mwezako tena mtumishi unayemjua, kwahiyo ni kuwa makini sana na kumuomba Mungu akuepushe na watu wenye nia mbaya.

Huyo kijana anayekufuatilia kila siku sitisha mazungumzo yake mapema kabla hamjafika mbali, unapoona kuna dalili ya kuzama kwenye zinaa na huyo mtu unayezungumzanaye Kataa hayo mazungumzo mapema…usijaribu kufanya kosa la kujilegeza kwake, hata kama ni mtumishi anayekufundisha..weka mipaka na mazungumzo yatakayokupeleka kwenye uasherati, kama anadai kukupenda aje kwako kwa heshima atake kukuoa na sio kuzungumza zungumza habari hizo bila utaratibu wa kiMungu.

Tutaikimbiaje zinaa 

Weka agano na macho yako kama alivyofanya mtumishi wa Mungu Ayubu.

Ayubu 31:1 Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?

Unapokutana na wanawake wamevaa kizinzi, usikodoe macho yako kumtazama, kijana amevaa kimtego usimtazame tazame, macho yako yatazame mbele bila kugeuka geuka

Mithali 4:25 Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.

Ukiingia mtandaoni kufuatilia taarifa za maana, au kufanya kitu fulani cha msingi ukakutana na hizo picha za uchi, usitazame mara mbili mbili wala usigandishe macho yako kutazama..KIMBIA, maana shetani anakutafuta akunase…usiseme acha nitazame tu kidogo hiyo ni sauti ya ibilisi, biblia inasema…

Mithali 6:28 Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue?

Usikubali kukanyaga vichocheo vya zinaa, maana ukikanyaga utaungua tu haijalishi we ni wa kiroho sana.

Tutaikimbiaje zinaa 

Halikadhalika mawazo ya zinaa yanapoingia ndani yako..usiipe nafasi hata kidogo, kataa hayo mawazo huko huko kwenye moyo wako mapema, acha kuwaza waza na kusikiliza mahubiri ya shetani, wakati mwingine ni vigumu kutokuwa na mawazo hayo kwasababu ya vitu tunavyovitazama na kuvisikia bila kutarajia.. lakini Bwana Yesu alisema…

Marko 7:15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu.

Hapa hazungumzii tu chakula, lakini pia na mambo yote yanayoingia ndani ya mtu aidha kwa kupitia macho au masikio, lakini kwasababu macho hayana pazia utaona tu watu wamevaa vibaya..sasa hilo sio tatizo, kosa ni pale unapoingiza hizo taswira kwenye moyo wako na kuanza kufikiria fikiria…hapo utajikuta unaanza kuzini moyoni mwako pasipo hata kukutana na huyo mtu.

Sasa ufanye nini? 

Unapokutana na hali kama hiyo…haraka sana Omba Roho Mtakatifu akusaidie kuondoa hiyo taswira na hiyo kumbukukumbu ndani yako, usikubali kabisa hayo mawazo yakae ndani yako hata saa moja maana yatakukunajisi… hivyo yakupasa ulie, uombe rehema na msaada wa Mungu. Na Roho Mtakatifu atakusaidia.

Huko ndiko kukimbia dhambi ya zinaa. 

Je,! Dada/kijana umeweza kukimbia zinaa kama biblia inavyosema? Hebu kupitia somo hili jitathimini maisha yako na Roho Mtakatifu akusaidie kuchukua hatua.

Kama hujaokoka, kumbuka kuwa huwezi kukimbia zinaa katika dunia hii, haijalishi utaombewa na kushauriwa vya kutosha!! Leo umekwisha fahamu ukweli kuwa ni wewe kuokoka kweli kweli na kujitenga na vichocheo vyote vya zinaa na kuomba kujazwa Roho Mtakatifu na kuweka Neno la Mungu kwa wingi ndani yako ndipo utakuwa salama kwenye hii dunia iliyoharibika.

Kumbuka wazinzi na waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu (1Wakoritho3:9) bali sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kibiriti soma Ufunuo21:8.

Tunaishi ukingoni mwa nyakati parapanda imekaribia na Yesu Kristo anarudi muda wowote.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *