
TWAWASIHI MSIIPOKEE NEEMA YA MUNGU BURE.
2 Wakorintho 6:1 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure”.
Tumepewa neema ya Mungu ili tuitumie na sio kukanayo tu bure, jambo ambalo watu wengi hawajui ni kwamba siku ile ya hukumu tutahukumiwa kwa kadri ya neema tuliyopewa, kwamba tuliitumiaje? (Sizungumzii hukumu ya waovu)
Ni vizuri kufahamu kuwa dhawabu za Mungu zitatolewa kulingana na neema mtu aliyopewa, na sio yale matendo aliyoyafanya..
Namaanisha kuwa na jina kubwa, kuheshimiwa na kukubaliwa na watu wengi sio kigezo cha kwenda kupokea dhawabu kubwa, bali ni kiwango cha neema uliyopewa ulitumiaje?
Unaweza ukawa hufanyi miujiza, hujulikani na watu, unahubiri injili ya Kristo kwa kusambaza tu vipeperushi mitaani, au kuwatumia watu mistari ya biblia, au kuwaombea watu waokoke, halafu dhawabu yako ikawa kubwa kuliko hata yule mtu anayejulikana na watu kuwa ni mtumishi mkubwa, kwasababu gani? Kwasababu Mungu hapokei uso wa mwanadamu anaangalia kiwango cha neema aliyompa mtu ameitumiaje?
Kwa mfano tuchukulie mtu mwingine amepewa asilimia 100 ya neema ya Mungu, mwingine akapewa asilimia 10, yule aliyepewa 100 akatumia asilimia 60 ya neema hiyo, na yule aliyepewa 10 akatumia asilimia yote kumi, ni rahisi kudhani huyu aliyetumia asilimia 60 ni mkubwa kuliko yule aliyetumia asilimia 10 yote kwasababu ya namba hizo, lakini ukweli ni kwamba huyu wa asilimia 10 ni mkuu kuliko yule wa asilimia 60… kwasababu kinachoangaliwa sio ukubwa wa namba bali ni kile ulichopewa na jinsi ulivyotumia.
Labda tuchukulie tena mfano huu uweze kuelewa vizuri, Mwanafunzi mmoja anaweza kupewa maswali 10 na kati ya hayo akapata 9 na kukosa 1..Wakati huo huo mwanafunzi mwingine anaweza kupewa maswali 100, akapata 60 na kukosa 40, kwa namna ya kawaida unaweza kusema yule wa maswali 100 ndiye aliyefaulu zaidi ya mwingine, lakini tukirudi kwenye asilimia utagundua kuwa yule aliyepewa maswali 10, ndiye aliyefaulu zaidi ya mwenzake, amefaulu kwa asilimia 90%..Ukilinganisha na yule wa maswali 100 yeye kafaulu kwa asilimia 60%. Ambayo ni ndogo.
Kama aliweza kuwa mwaminifu katika maswali 10 basi atakuwa mwaminifu katika maswali 100, ndivyo ilivyo na kwetu sisi, kila mmoja kapimiwa kipimo chake cha neema, je unaitumiaje hiyo neema? Tunasoma Bwana mmoja katika biblia aliwapa watumwa wake talanta kila mmoja talanta yake, wakafanye kazi..lakini baadaye aliporudi akataka apewe hesabu kamili, na mtumwa mmoja aliyepewa talanta moja yeye akaidharau akaenda kufukia chini wakati wengine wameenda kufanya kazi na kuleta faida, mwisho wa siku yule Bwana akasema maneno haya ambayo yanatufundisha na sisi jinsi tunavyoitumia neema ya Mungu. Tunasoma
Mathayo 25:14-30 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
[15]Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
[16]Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.
[17]Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
[18]Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
[19]Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
[20]Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
[21]Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ULIKUWA MWAMINIFU KWA MACHACHE, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
[22]Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.
[23]Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ULIKUWA MWAMINIFU KWA MACHACHE, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
[24]Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
[25]BASI NIKAOGOPA, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
[26]Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe MTUMWA MBAYA NA MLEGEVU, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
[27]basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
[28]Basi, mnyang’ anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
[29]Kwa maana KILA MWENYE KITU ATAPEWA, NA KUONGEZEWA TELE; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang anywa.
[30]Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Angalia leo neema ya Mungu uliyopewa unaitumiaje au umepokea tu bure kama huyu mtumwa mlegevu?. Ulipewa neema ya kuombea kanisa la Kristo unaitumiaje hiyo neema? Ulipewa neema ya kusambaza vipeperushi au kuposti maneno ya Mungu mtandaoni je unaitumiaje hiyo neema? Ulipewa neema ya kukusanya umati mkubwa na kuhubiria injili ya kweli je! unaitumiaje hiyo neema au unatumia kwa masilahi yako tu? Neema ya Mungu uliyopewa kuchangia kazi ya Mungu kwa mali ulizobarikiwa unaitumiaje? Neema ya Mungu uliyopewa kumwimbia Mungu na kumsifu unaitumiaje au ni mpaka usukumwe sukumwe au kualikwa? Neema ya Mungu uliyopewa kusoma biblia, kuomba na kufunga unaitumiaje? Angalia nafasi yako ni ipi kwenye mwili wa Ktisto (kanisa) na unaitumiaje? Fahamu kuwa hakuna upendeleo kwa Mungu na wala Mungu hadharau kile kidogo alichompa mtu zaidi sana anaangalia huyo mtu ameitumiaje? Sasa kama Mungu hakudharau kwanini wewe unajidharau na kuona haufai kuitwa mtumishi wake kwa kile kidogo ulichopewa? Fahamu kuwa kwa Mungu hakuna mtumishi mkubwa wala mdogo, wote ni watumishi..hata yule anayefagia kiwacha cha kanisa ni mtumishi wa Mungu sawa na yule nabii au yule mchungaji, kinachotutofautisha ni neema tu mtu aliyopewa na huduma/karama aliyopewa lakini kila mmoja atalipwa sawa na uaminifu wake katika kutumia neema ya Mungu.
2Wakorintho 6:1 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
Maran atha (Bwana Yesu anarudi)
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.