
ATI! HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA MUNGU.
Jina kuu lipitalo majina yote, jina la Yesu Kristo wa Nazarethi litukuzwe vizazi vyote, karibu tena katika siku ya leo tutanue fahamu zetu kwa kujifunza elimu ya ufalme wa Mungu.
Biblia inasema shetani ni muongo na ni baba wa huo (Yohana8:44), maana yake yeye ndiye mwazilishi wa uongo, alipomwendea Hawa pale bustanini alimtumia nyoka kumlaghai, na alijifanya kama hajui mambo, ingawa alikuwa anafahamu kabisa ukweli wote, lakini alijifanya hajui ili ampate Hawa kirahisi na amwingize kwenye uongo wake. Hivyo akamwambia…
Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. AKAMWAMBIA MWANAMKE, ATI! HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA MUNGU, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
[2]Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;
[3]lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.
[4] NYOKA AKAMWAMBIA MWANAMKE, HAKIKA HAMTAKUFA,
[5]kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, NANYI MTAKUWA KAMA MUNGU, MKIJUA MEMA NA MABAYA.
Sasa tuangalie vizuri hiyo kauli “ATI! HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA MUNGU?
Sasa kwanini aseme hivyo ilihali anajua ndivyo ilivyo, kwasababu ni kweli ndivyo alivyosema Mungu ukirudi ile sura ya pili (Mwanzo 2:16-17), kauli hiyo inampa shetani nafasi ya kusema jambo kwa Hawa ambalo ndio tageti yake..na ndio maana alijifanya kama hajui vizuri akamwambia “ati hivi” yaani ni kama mtu hana uhakika na kile anachokifahamu, kwahiyo anataka umthibitishie, na unaona anasema ati hivi ndivyo alivyosema Mungu msiyale matunda ya miti yote, na anafahamu kabisa kwamba Mungu hakusema msiyale matunda yote yaliyopo bustanini, bali mle matunda yote isipokuwa matunda ya mti wa katikati ya bustani, kwahiyo huyu nyoka ni kama anageuza geuza ukweli halisi, kwanini afanye hivyo? Ni ili ampe Hawa kunyosha ukweli wote na baada ya hapo aseme uongo wake mkamilifu. (Kumbuka hayo siyo mawazo ya nyoka lakini ni ibilisi nyuma yake kama vile alivyomvaa Petro kwa mawazo, akaanza kumfariji Bwana Yesu kwamba hautapitia mateso ya msalaba wakati Bwana alikuwa ameandikiwa hayo, lakini yeye Bwana Yesu alitambua hayo mawazo sio ya Petro ni shetani nyuma yake kwasababu yanapingana na Neno la Mungu, hivyo akamkemea shetani saa hiyo hiyo ndani ya Petro (Mathayo 16:23)
Lakini Hawa yeye hakutambua alidhani ni nyoka tu anazungumza, na huyu nyoka sio huyu tunayemwona leo akitembea mavumbini, nyoka kabla hajawa kama leo alikuwa ni mnyama mwerevu sana kuliko wanyama wote, pengine alikuwa anakaribiana na mwanadamu ukimtoa yeye anafuata labda sokwe mtu, na huwenda alikuwa kama mtumishi wa Adamu na Hawa kusaidia kazi ngumu ngumu… lakini baada ya shetani kumtumia kuwadanganya Adamu na Hawa baadaye alilaaniwa na Mungu ndio akawa kama hivi leo… lakini hukuwa hivi tangu Mwanzo..soma Mwanzo 3:14 utathibitisha.
Kwahiyo baada ya Hawa kutiririka kusema ukweli wote kwamba ndivyo tulivyoagizwa tule matunda ya miti yote ya bustanini…lakini tusile wala tusiyaguse matunda ya mti ulio katikati ya bustani…kwa maana siku tukiyala tutakufa, hapo hapo shetani akapata nafasi ya kusema uongo wake, akamwambia ”hakika hamtakufa” kumbuka Mungu alikwisha kusema “hakika mtakufa (Mwanzo 2:17).
Sasa haishii tu hapo kwasababu alijua Hawa asingekubali kuingia mtegoni kirahisi rahisi, akaongeza na sababu kwanini waliambiwa wasile hayo matunda, sababu ambayo Hawa hakuwahi kujua, akamwambia..
Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
[5] KWA MAANA MUNGU ANAJUA YA KWAMBA siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
Kwahiyo Hawa aliposikia hivyo, habari ya kuwa kama “MUNGU” masikio yake yakawasha, akatamani kujua zaidi, huwenda akaendelea kusikiliza mahubiri ya nyoka kwa kitambo kidogo mpaka baadaye akajikuta amehama kabisa katika ule msimamo aliokuwanao, akaanza kutamani walau aonje hata kidogo ili adhibitishe alichokisikia kwa nyoka, hivyo akayatwaa hayo matunda akala (pengine walikula wote na nyoka, biblia haijafafanua zaidi, lakini naamini hivyo), na baadaye akampa na mumuwe, baada ya hapo wakajikuta fahamu zao zimebadilika, wakajikuta ni kama wamejitambua hivi, kwanza wakajiona wapo uchi, wakaona aibu kubaki vile vile. Sio ajabu hata leo watu wanatembea uchi lakini hawaoni aibu!! ni kwasababu fahamu zao zimepigwa.
Kwahiyo baada ya Adamu na Hawa kufunguliwa fahamu zao kilichobaki ni kukimbia kutafuta sehemu ya kujistiri, wakakimbilia vichakani wakajichonea majani kustiri viungo vyao, maana haifai tena kubaki vile, ni kama mtoto mchanga ambaye hajajitambua, tuchukulie mfano apewe ufahamu wa mtu mkubwa, bila shaka atakimbia kujificha au kutafuta mavazi afunike uchi wake maana tayari amepata ufahamu, amefumbuliwa macho. Ndicho kilichowapata wazazi wetu Adamu na Hawa, macho yaliyofumbuliwa sio haya ya damu na nyama bali ni ufahamu wao ulifunguliwa, na kweli baada ya hapo walijua mema na mabaya kama nyoka alivyowaambia, lakini kujua mema na mabaya matokeo yake ni kufukuzwa na Mungu na kulaaniwa.
Mwanzo 3:22-24 BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, KWA KUJUA MEMA NA MABAYA; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;
[23]kwa hiyo BWANA Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.
[24]Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.
Kwahiyo shetani akawa amefanikiwa namna hiyo, lakini alianza kama mjinga kwa kusema ATI! HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA MUNGU?
Sasa shetani bado ni yule yule hajabadilika, tena siku hizi ameshawasoma wanadamu kwa muda mrefu, hivyo anajua mbinu nyingi za kuwadanganya. Na haji kama yeye, anawatumia watu walio kama wewe, kama alivyomtumia nyoka.
Kumbuka hatafuti watu walio mbali na Mungu, zaidi sana anawatumia hao kukuangusha wewe uliye karibu na Mungu. Sasa jiulize, Hawa alikuwa mkamilifu kabisa lakini bado alidanganywa, je mimi na wewe ambayo tulizaliwa katika dhambi si zaidi kudanganywa tusipokuwa makini?
Leo hii we ni binti uliyeokoka kweli kweli, na kijana anakufuata anakuambia ati hivi ndivyo alivyosema Mungu tusiwe na mahusiano ya kimapenzi? Na wewe unaanza kutiririka kumuelezea kila kitu, pasipo kujua kuna mahali shetani anataka kukufikisha. Kwanini asimfuate mtumishi wa kiume aulize swali hilo, na yeye mwenyewe anajua kuwa na mahusiano hayo nje ya ndoa ni dhambi.
Mwingine anaambiwa “ati hivi ndivyo alivyosema Mungu”…tusijipambe kwa nje? Ati hivi ndivyo alivyosema Mungu suruali ni vazi la kiume? Ati hivi ndivyo alivyosema Mungu kujichua ni dhambi? Ati hivi ndivyo alivyosema Mungu pombe ni dhambi?
Ukisikiliza maswali ya namna hiyo… mwisho wa siku utahamishwa na kubadilishwa kabisa, kwani shetani ni yule yule anatafuta kukuingizia maarifa fulani ili uanze kuchanganyikiwa na kuona kama ulichosikia ni ukweli fulani, kumbe ni ukweli uliochanganyikana na mauti.
Watu wengi wamepigwa ufahamu kwa njia hii, wanapewa tu ukweli kidogo..wao pasipo kusimama katika maagizo ya Mungu (Neno la Mungu), wanajikuta hata Imani wameacha, wamehamishwa mbali, wengine wamefungiwa makongwa wakaacha kusikiliza Roho Mtakatifu, wakaingizwa kwenye mapokeo, ndio maana wengine hawamwabudu tena Mungu katika Roho na kweli wanaabudu siku, mwezi, wengine wamepigwa fahamu zao hata wanaogopa kula vyakula vilivyotakaswa na Mungu, wengine kuvaa nguo ya rangi fulani, au kutumia vyombo vyenye maua fulani, n.k n.k. Hayo ni mafundisho ambayo yanatoka moja kwa moja kwa ibilisi, lakini yanakuja kwa mafumbo mafumbo.
Jihadhari sana na mafundisho hayo yasiyo na msingi wa Neno la Mungu, bali msingi wake ni ndoto na maono, au elimu ya kuteka fikira kwa kutumia biblia ndivyo sivyo.
Na hapa ndipo unahitaji kuwa karibu sana na Mungu kwa kusoma Neno lake sana, kutafuta maarifa sahihi kwa watumishi wa kweli, kuomba kujazwa Roho Mtakatifu kila siku. Roho Mtakatifu atakutia katika kweli yote na atakufunulia njia sahihi na njia ya upotovu.
Yohana 16:13Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.
Tunaishi ukingoni mwa nyakati sana, unyakuo umekaribia sana. Hivyo kama bado hujaokoka kweli kweli fahamu kuwa umechelewa sana, ni heri leo utumie hii nafasi moja kumpa Yesu maisha yako.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.