
LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA
1 Wakorintho 2:12 “Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.”
Kuna roho ya dunia ambayo ndiyo inawafanya watu wawe wa kidunia, ukiona leo watu kanisani wanaenda kama wanaenda disco, wanavaa jinsi makahaba wavaavyo, wamejipodoa kama majini, ujue ni ile roho ya kidunia imo ndani yao inawafanya wawe hivyo.
Kila kitu mtu anachokipenda kuna roho inamsukuma apende, hivyo angalia unapenda nini? Neno la Mungu linasema tusiipende dunia (1Yohana2:15), ukiona unapenda dunia, unapenda raha zake, unashabikia vitu vyake, unaiga namna yake basi ujue umepokea roho ya dunia ijapokuwa unasema umeokoka na unanena kwa lugha.
Angalia leo ni roho gani imo ndani yako? Ukiwa na Roho wa Mungu (Roho Mtakatifu) atakufanya kuwa wa kiMungu, utapenda utakatifu kwakuwa yeye ni Mtakatifu, utachukia udunia kwa kuwa yeye sio rafiki wa dunia (Yakobo 4:4), atakufanya upende kusoma Neno la Mungu, atakufanya upende kuwa uombaji, atakusukuma upende kuwashuhudia wengine, atakufanya upende kwenda ibadani, atakufanya upende kuvaa kwa kujistiri na kuwa na adabu, kwa ufupi Roho Mtakatifu atakufanya uwe wa Mungu kwasababu ni Mungu mwenyewe. Lakini roho ya dunia ni roho ya ibilisi na kazi yake ni kuwafanya watu wawe wa yeye.
Swali ni lile lile je ni roho gani umepokea?
“Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu”.
Bwana Yesu akubariki.
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618.