
NAWE UJITAHIDI
2 Samweli 5:24 “Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti.
Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze neno la Mungu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119’105).
Kuna mambo ambayo Mungu hawezi kufanya kama mtu asipoweka kwanza bidii/nia ya kuhitaji msaada wa Mungu, haijalishi huyo mtu ataombaje!!
Kwa mfano unaomba Mungu akuinue kimaisha, akupe baraka za kimwili halafu we unabaki tu kuomba hauweki bidii kufanya kazi yoyote ya halali, hapo utaomba sana na kuombewa lakini hakuna huo muujiza wa kubarikiwa ukiwa umelala kitandani kusubiria!! Ni lazima uamke ukajishughulishe kufanya kazi kwa mikono yako ndipo sasa Mungu abariki kazi ya mikono yako.
Lakini ukiwa mvivu, unaomba tu na kukaa, hapo unaweza ukasubiri sana na ukaona Mungu hajibu au hakupendi! Lakini Mungu anakujali na tayari ameshakubariki kama umekwisha fanyika mtoto wake, (namaanisha kama umezaliwa mara ya pili), anachosubiri tu ni wewe uamke na kufanya kazi yoyote kwa mikono yako, hata kama ni kazi ndogo kiasi gani, kinachohitajika ni jitihada zako tu Mungu yupo kukuinua na kukubariki zaidi.
Vivyo hivyo katika mambo ya rohoni, ni kujitahidi, sio kutaka tu au kutamani halafu huonyeshi juhudi kutekeleza.
2 Wakorintho 8:11-12 “Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutaka, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo.
[12]Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo”.
Acha hiyo tabia ya kusubiri subiri, amka omba, weka mipango ya kusoma biblia na uanze kutekeleza, acha hiyo tabia ya kusema wengine wamepewa neema zaidi yako, ni vizuri kufahamu kuwa neema ya Mungu inafanya kazi pamoja na wewe unavyoonyesha juhudi, kwa mfano ukisema kuanzia leo nitaamka kila alfajiri na kuomba, au usiku wa manane na kusoma biblia na ukajitahidi kweli kufanya hivyo ukashinda mwili wako, ndipo utashangaa kuna nguvu ambayo hata hujui imetokea wapi inakusaidia, kama ulikuwa umezoea kuomba tu dakika tano haizidi kumi, ukasema leo nitaomba lisaa limoja, ukapambana kweli hata kama mwili hautaki ukaomba hivyo hivyo nataka nikuambie ni swala la muda tu kuna nguvu inaachiliwa juu yako unashangaa unaomba bila kuichiwa maneno, unashangaa unasoma biblia mpaka sura kumi wakati ulikuwa unasoma tu moja unachoka, hivyo ndivyo neema inavyofanya kazi kutusaidia… ndio maana tumepewa Roho Mtakatifu kama msaidizi sio mfanyaji ni msaidizi, tusipoweka jitihada kufanya yeye anatulia tu kukusubiria.
Kwahiyo leo amka anza kuweka bidii ya kujizoeza utauwa, weka jitihada ya kuomba hata kama hauna maneno omba hivyo hivyo ndio kujizoeza kwenyewe, na uzuri ni kwamba ukishajizoeza kuomba kwa masafa marefu.. siku ukiomba nusu saa unaona ni kama vile hujaomba, na mambo mengine ya kiroho ni kujitahidi.
Unakarama ya kuimba na kumsifu Mungu jitahidini kuimba usiseme suati ni mbaya we imba hivyo hivyo Roho Mtakatifu atakuboresha, lakini ukikaa tu na kusubiria neema ikushukie haiji kwa namna hiyo, weka jitihada tafuta wengine wakusaidie, kama ni kushuhudia anza na marafiki zako washuhudie, endelea kuonyesha jitihada na Mungu sasa atakusaidia, lakini pia utakatifu ni kujitahidi kwa bidii, usikae tu ukasema utakuwa mtakatifu kimiujiza, hilo jambo halipo!! Ni lazima we mwenyewe uweke bidii ya kutafuta, ni lazima ujitenge na dhambi kwa gharama yoyote ile, ni lazima ujitenge na udunia,ukae mbali na makundi ya watu wabaya. Huwezi kuomba Mungu akusaidie uwe mtakatifu halafu bado unashikilia dhambi kwa mikono yako, bado unatazama vitu visivyofaa kwenye simu yako..hapo utaomba sana lakini kuwa mtakatifu ni vigumu sana mpaka ujitenge na maisha hayo ya uchafu.
Amua leo kuweka juhudi ya kumtumikia Mungu na Mungu atakusaidia.
Maran atha!.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.