
MUNGU WETU NI MUNGU WA UMOJA
Warumi 15:5-7 “Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie KUNIA MAMOJA ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu;
[6]ili kwa MOYO MMOJA na kwa KINYWA KIMOJA mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
[7]Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe”.
Kati ya jambo ambalo Mungu anatamani sana kuona kwa watoto wake ni kitu kinachoitwa UMOJA, umoja ni jambo kubwa sana analolitazama Mungu aweze kutubariki, ni jambo linalofuta uwepo wa Mungu kwa haraka sana, na ndiyo Kristo alituombea kwa Baba tuwe na umoja.
Yohana 17:20-21 “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.
[21]Wote WAWE NA UMOJA; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma”.
Hapo anasema wawe na umoja kama wewe ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, maana yake Kristo na Baba walikuwa na umoja, sehemu nyingine alisema mimi na Baba tu umoja (Yohana 10:30),
Yohana 17:22 “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.
Tangu mwanzo, Mungu alikuwa ni Mungu wa umoja, ijapokuwa yeye mwenyewe anao uwezo wa kufanya kila kitu peke yake bila kusaidiwa, lakini utaona alipokuwa katika kufanya kazi yake ya uumbaji alikuwa hafanyi mwenyewe, alikuwa anashirikiana na malaika zake aliowaumba awali, tunasoma..
Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi”.
Hapo anasema ”tumfanye mtu” japokuwa yeye ndiye aliyeumba kwa mikono yake lakini hilo wazo lake alishirikisha kwanza malaika wake, hata wakati ule Bwana alipoharibu ule mnara wa Babeli hakushuka mwenyewe, alisema
“Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao”. (Mwanzo 11:7), lakini pia ukisoma biblia vizuri utaona sehemu nyinyi Mungu alikuwa anajishusha sana na kujiweka katika hali ya ubinadamu ili tu kutufundisha kuwa yeye ni Mungu wa umoja, mfano sehemu nyingine alikubali kushauriwa na Musa alipotaka kuangamiza wana wa Israeli wote kwa makosa yao, lakini Musa akamtuliza hasira yake. (Kutoka 32:10-12).
Unaona jinsi Mungu anavyopendezwa na umoja!!
Ukweli ni kwamba hatuwezi kumpendeza yeye kama sisi wenyewe hatuna umoja, kama hamna umoja ndani ya kanisa, Mungu hayupo ndani ya hilo kanisa haijalishi ni kubwa kiasi gani, kama hakuna umoja ndani ya familia, Mungu hawezi kuwepo hapo haijalishi mtaomba kiasi gani, hata katika kuhubiri injili kama hatuna umoja watu hawezi kuamini, kinachowaminisha watu wasioamini ni pale wanapotuona kwanza tuna umoja na sio miujiza mingi na maneno mengi mengi yasiyo na umoja.
Yohana 17:21 “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma”.
Tafuta umoja na amani leo ili umuone Mungu, we ni mama jichuche kwa mume wako acha kiburi, we ni baba kuwa na ushirika na familia yako acha kufanya mambo kifyako fyako, we ni mchungaji kuwa na umoja na washirika wote, acha tabia ya kubagua na kupendelea, we ni mshirika kuwa na umoja na wapendwa wenzako, acha kuangalia madhaifu ya wengine na kuhukumu, acha kujitenga, acha ubinafsi, tutafute umoja! Tutafute amani na watu wote!! Tusimpe ibilisi nafasi!!
Mungu atubariki sote. Amina.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.