
HATUNA NIA NYINGINE.
Wagalatia 5:10 “Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote”.
Nia yetu ni kumtafuta Bwana kwa mioyo yetu yote, na hatumtafuti kwasababu tunataka mambo yetu yaende sawa, hatumtafuti kwasababu tunataka tubarikiwe.. tuwe na maisha mazuri, hatuendi kanisani ili tupate wachumba, au tutimize matakwa yetu, hatusomi biblia ili wachawi wasituloge, hatuombi ili tupate mahitaji tu basi, hatumsifu ili watu watuone, hatumtolei ili tupokee zaidi au mambo yetu yaende, hatuhubiri ili tupate pesa au tukalipwe mbinguni..ndio tunajua zipo thawabu zetu lakini hatujishugulishi na kazi ya Bwana kwa nia ya namna nyingine, kwa ufupi hatumtafuti Mungu kwa sababu sababu, Bali tunamtafuta kwanza kwasababu tunampenda, yeye ni Baba yetu na sisi ni wanae, na kama vile baba amtunzavyo mwanae, ndivyo Baba yetu anavyotutunza na kutuhudumia katika mambo yote na hakuna wa kutudhuru kwa jambo lolote lile..
Lakini pia mahusiano yetu si ya baba na mtoto tu, ila pia tunamahusiano naye kama mke na mume, yeye amekuwa kama Bwana wetu na sisi ni wake zake hivyo mahusiano yetu ni yale ya kindoa, mahusiano haya huwa hayana sababu sababu bali ni watu wanapendana tu basi ..ndio maana biblia inasema..
“..Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu.
[7]Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; KAMA MTU ANGETOA BADALA YA UPENDO MALI YOTE YA NYUMBANI MWAKE, ANGEDHARAULIWA KABISA.”(Wimbo8:6-7
Unaona jinsi upendo ulivyo na nguvu, leo hii watu wanaachana kwenye ndoa kisa uchumi umekuwa mgumu, hamna fedha, hamna hiki na kile… ukiona hivyo ujue ya kuwa hao watu aidha kuna mmoja aliingia tu kwenye ndoa kwasababu ya faida zake tu na sio kwamba amempenda mwezake kwa moyo kabisa.. huwenda ni tamaa zake tu, lakini upendo wa kweli hauna sababu sababu..wala fedha, Mali na kitu chochote kilichotukuka duniani haina nguvu zaidi ya upendo.
Na ndivyo pia ilivyo kwa Bwana wetu Yesu, hatumpendi tu kwasababu sababu, hatumtafuti ili tupate tu vitu..bali kwasababu tunampenda na hata tukikosa vitu vyote, au tukipitia magumu kiasi gani bado tunampenda, na kwasababu hiyo yeye ndiye aliyetupenda kabla yetu..na hivyo hawezi kutuumiza hata kidogo, anasema hakuna wa kututenga na upendo wake.
Warumi 8:35-38 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
[36]Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
[37]Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, KWA YEYE ALIYETUPENDA.
[38]Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
[39]wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.
Upendo unaozungumziwa hapo sio wa sisi kumpenda Bwana, bali ni yeye kutupenda sisi hakuna wa kututenga nao, sisi tunaweza kumwacha kutokana na sababu zetu lakini yeye hawezi kutuacha kamwe.
Bwana Yesu ni mpenzi wetu haswa, mahusiano ya hapa duniani yamewekwa tu kama somo kutufundisha jinsi Bwana anavyotupenda…na jinsi na sisi tunapaswa tumpende.
Lakini ikiwa kuna mtu anakuelekeza kwake kwa nia yake mwenyewe, anakufundisha habari za Mungu ili akutumie kwa sababu zake mwenyewe na wewe hujui, basi mtu huyo atachukua hukumu yake mwenyewe biblia inasema hivyo.
Je! Bwana Yesu ni Bwana wako kweli? Unampenda kwa moyo wako wote? Una nia nzuri na yeye? au upo na nia ya namna nyingine!!
Bwana atuongezee neema yake ili tuzidi kumpenda na kumtafuta kweli kweli .
Kumbuka amekaribia kurudi sana!!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.