
NA HAO WALIO WA KRISTO YESU WAMEUSULIBISHA MWILI PAMOJA NA TAMAA ZAKE.
Wagalatia 5:24 “Na hao walio wa Kristo Yesu WAMEUSULIBISHA MWILI pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
[25]Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Kusulubisha mwili ni kufanyaje? Kwanza tufahamu maana ya kusulibisha?
Kusulubisha ni kuadhibisha kwa kuning’iniza kwenye mti wa msalaba, au nguzo iliyonyooka, kwa kufungwa au kugongelewa miguu na mikono, na kuacha hapo mpaka ufe. Kwahiyo ni adhabu ya mateso makali sana, ndiyo iliyokuwa inatolewa zamani kwa watu waliopatikana na makosa.
Sasa, hapo biblia inasema hao walio wa Kristo Yesu WAMEUSULIBISHA MWILI pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Maana yake wameutesa na kuua mwili kwa mfano wa mateso ya kusulibisha.
Jambo la kwanza kabisa mtu analopaswa kufanya baada tu ya kuingia katika wokovu ni kusulibisha mwili wake pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake zote..ili Roho Mtakatifu apate nafasi ya kumtengeneza mtu huyo, lakini watu wengi wameshindwa na tamaa za mwili kwasababu gani? Hawajakusudia kumpa Roho Mtakatifu nafasi ya kuwatengeneza, hawajataka kusulubisha miili yao..hivyo wanaishia tu kutumikishwa na tamaa za mwili kama uasherati, ulevi, madawa ya kulevya, uvaaji mbaya, anasa n.k (wanabakia kuwa wakristo vuguvugu).
Sasa tunasulubishaje mwili pamoja na tamaa zake mbaya? Hakuna njia nyingine ya kusulibisha isipokuwa ni kwa kuutesa, kwa kunyima zile raha zake na tamaa zake, mfano mwili siku zote hautaki mambo ya rohoni kama kuomba, kufunga, kukesha, n.k unataka tu ulale usiku kucha au usilale lakini ukeshe kutazama vichekesho na kuburudika, unataka tu kula masaa yote hautaki kusikia kabisa habari ya kufunga hata siku moja kwa week, Bwana Yesu alisema “roho i radhi lakini mwili ni kikwazo”, hivyo ni kuulazimisha tu kufanya mapenzi ya Mungu.
Unalazimisha kufunga hata kama utakuletea sababu sababu usisikilize … mwanzoni utaona kama unaishiwa nguvu lakini we songa mbele ni udanganyifu wa mwili usikubali kusikiliza sauti zake…isemeshe mwambie leo hakuna kula mpaka masaa 24..huko ndio kuusulibisha, lakini sio kuacha tu kula basi, hapana unakuwa na ratiba ya kuomba pia..unapoomba Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kukujenga na kukutia nguvu.
Hivyo tengeneza ratiba yako ya kuomba kila siku, iwe ni usiku au alfajiri amka omba.. usiruhusu mwili ukulalishe usiku wote, amka omba..jilazimishe, tena ukiona bado unakuletea usingizi jimwagie maji ya baridi au toka nje kwenye baridi… mwanzoni utaona ugumu lakini kadri unavyoendelea baada ya muda mfupi usingizi wote utaondoka na unajikuta unazama rohoni mpaka baadaye unakuja kushangaa umeomba masaa ya kutosha.
Pia mwili unapenda kulishwa na burudani burani kama vichekesho-vichekesho visivyo na maana, vitamthilia, picha picha za uchi, hadithi hadithi za mapenzi, ni chakula kizuri cha mwili hivyo unapiga marufuku, unafuta vyote kwenye simu yako, unaweka agano na macho yako. Kama ulikuwa umezoea kulisha vyakula hivyo..mwanzoni utakusumbua, utakushawishi sana, utakuambia tazama hata kidogo ..mara moja tu, lakini wewe usisikilize sauti yake, jizuie na vitu hivyo, kama ni madawa ya kulevya ni vivyo hivyo jizuie…jitese, ukifanya hivyo ukatii maamuzi yako nakuambia ni muda mfupi tu tamaa zote za mwili unasahau. Lakini hili linawezakana kwa wewe kuamua kusulibisha mwili wako na kukataa tamaa zake zote..hauwezi kusema unataka kushindana na mwili kama bado unaubembeleza mbeleza.
Huko ndiko kusulibisha mwili, je umeusulibisha mwili wako pamoja na tamaa zake??
1 Wakorintho 9:24-27 “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.
[25]Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.
[26]Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;
[27] BALI NAUTESA MWILI WANGU NA KUUTUMIKISHA; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”
Maran atha.(Bwana Yesu anarudi)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.