
SISI NI WARITHI WA BARAKA ZA MUNGU
Wagalatia 4:1 “Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
[2]bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
[3]Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.
[4]Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,
[5]kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
[6]Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.
[7]Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”
Sifa nyingine ya mtoto ni kurithi mali za baba yake, na hakuna baba anayeacha urithi kwa watoto wasio wake hata kama alikuwa na ukaribu kiasi gani kama sio damu yake ni vigumu sana kumuachia urithi.
Kwahiyo tunaweza kusema mali alizonazo mzazi ni mali za watoto wake, ingawa mzazi akiwa hai bado, mtoto hana uhuru na mali za baba yake…hawezi kujichukulia tu atakavyo kwasababu ni za baba yake na ni za kwake baadaye, vinginevyo atakuwa kama yule mwanampotevu aliyechukua urithi kabla ya wakati akaenda kupata shida. (Luka 15:16)
Hivyo wakati mtoto awapo bado mtoto anakuwa kama mtumwa ingawa ni bwana wa yote…anakuwa anatumikishwa kwasababu yeye ni mtoto na hajajitambua bado. Tuchulie mfano huu tuweze kuelewa..
Wewe ni mfanyakazi katika nyumba fulani, bosi wako akakuachia familia uwatunze watoto wake..kinachofanyika ni kwamba wale watoto wanakuwa kama watumwa wako, wewe ndio unawapangia waishije, wafanye nini, wale nini, waende wapi, wasiende wapi kwa ufupi wapo chini yako haijalishi wazazi wao wana mali nyingi kiasi gani..wanapaswa waishi kama watumwa wako ingawa si watumwa bali wewe ndio mtumwa kwenye hiyo familia. (Kumbuka sizungumzii utumwa wa kidikiteta).
Vivyo hivyo na sisi, biblia inasema tulipokuwa watoto tulikuwa tukitumikishwa na KAWAIDA ZA KWANZA ZA DUNIA, mpaka Roho Mtakatifu alivyoingia ndani yetu akatushudia kuwa sisi ni watoto wa Mungu, na kama ni watoto wa Mungu basi ni warithi wa baraka za Mungu… hivyo hatupaswi tena kuishi kama watumwa.
Kuishi kama mtumwa ni kuishi kwa hofu ya maisha haya, kwamba kesho itakuwaje..nitaishije?, watoto wakiumwa nitapataje fedha ya matibabu? Nikiwa na familia kubwa nitawahudimiaje na mimi sina kipato kikubwa, ukishakuwa hivyo unakuwa chini ya KONGWA zito la mawazo na hiyo ndio kawaida ya dunia, hivyo hatupaswi kuwa hivyo Iwapo tumefanyika kuwa watoto wa Mungu. Tunapaswa tumchukulie Mungu kama Baba ambaye ni tajiri sana, kusema hivi haimaniishi kutofanya kazi au kutoweka malengo ya kesho hapana, hapa nazungumzia ile hali ya kusongwa na mawazo na kutaabika sana kana kwamba vitu unavyotaabikia ndiyo vinashikilia maisha yako.
1 Wakorintho 13:11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, NIMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO.
Ukiona ya kuwa una hofu sana ya maisha haya..basi fahamu kuwa umepungukiwa Roho Mtakatifu au umemzimisha, kwasababu anasema..
“… hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
[16]Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;
[17] NA KAMA TU WATOTO, BASI, TU WARITHI; WARITHI WA MUNGU, WARITHIO PAMOJA NA KRISTO; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
Ishi kama mrithi wa Mungu, tumeandaliwa makao mapya, tumeandaliwa mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, masumbufu ya dunia yasikusonge mpaka ukasahau we ni nani!! Tunaishi ukingoni sana tumekaribia kupokea urithi wetu wote.
Shalom.. Bwana Yesu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.